CHAMA cha Madaktari wa Wanyama (TVA) kimefanikiwa kutoa chanjo kwa wanyama mbalimbali dhidi ya magonjwa ya sotoka na kichaa cha mbwa sambamba na kufanya uchunguzi na matibabu kwa wanyama.
Hatua hiyo ni kuelekea maadhimisho ya Siku ya Madaktari wa Wanyama duniani,
Katibu wa chama hicho Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Meneja wa Kituo cha TVLA Iringa, Dk Geoffrey Mbata amesema ugonjwa wa sotoka unawapata mbuzi na kondoo na chanjo kwa mbwa na paka ni dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa.
“Mwaka huu maadhimisho haya hufanyika Aprili 27, mkoani Iringa na kaulimbiu yetu ni Madaktari wa Wanyama ni wahudumu muhimu wa afya hivyo tumekuwa na shughuli mbalimbali za kuadhimisha siku hii katika maeneo ya Wilaya ya Iringa, Wilaya ya Kilolo na Halmashauri ya Iringa,” ameeleza.
Dk Mbata amesema kuwa kuna umuhimu wa kuchanja wanyama kwani inadhibiti ueneaji wa magonjwa ili kupata mazao bora, salama na yenye afya kama vile mayai, maziwa na nyama.
Amesema kutokana umuhimu huo ni lazima kutoa matibabu na chanjo kwa wanyama.
“Tunafanya upasuaji mdogo kwa wanyama kama vile utoaji wa kizazi kwa mbwa na paka na huduma hizo zimefanyika bure kwa wafugaji wa maeneo husika,” amesema Dk Mbata.
Amesema huduma hizo hutolewa na madaktari wa wanyama, madaktari wasaidizi na kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ikiwemo Shirika la Chakula Duniani (FAO).
Pia amesema wanatoa elimu na hamasa kwa wanafunzi juu ya umuhimu wa uwepo wa madaktari wa wanyama nchini na duniani.
Ameeleza kuwa lengo la kuwepo kwa maadhimisho hayo ni kueleza umuhimu wa madaktari wa wanyama kwani jamii haitambui umuhimu wa madaktari hao.
“Tumetembelea shule tatu za manispaa ya Iringa kueleza umuhimu wa madaktari wa wanyama katika udhibiti magonjwa,” amesisitiza.