Mamlaka za Ujerumani zimetangaza kuwa kitengo cha ujasusi cha kijeshi cha Urusi (GRU), kinachofahamika kama kitengo 29155, kimefanya mashambulizi ya mtandao dhidi ya Walengwa mbalimbali barani Ulaya na kote ulimwenguni.
Ofisi ya Shirikisho la Ulinzi wa Katiba (BfV) ya Ujerumani ilisema kuwa Kitengo hicho kimehusika na mashambulizi dhidi ya miundombinu ya kiraia na shughuli za kijasusi katika Nchi za NATO na Umoja wa Ulaya (EU).
Aidha BfV ilibainisha kuwa kitengo hicho cha GRU kilifanya mashambulizi makubwa ya mtandao nchini Ukraine mwezi Januari 2022, muda mfupi kabla ya uvamizi kamili wa Urusi ulioanza Februari mwaka huo na Mashambulizi hayo yaliathiri miundombinu muhimu ya kiraia kama vile Huduma za Afya, Kilimo, na Shule, ikijaribu kuharibu kabisa mifumo ya Kompyuta inayohusika na Huduma hizo.
Wiki iliyopita, Marekani iliwashtaki Wanachama watano wa kitengo 29155 na Raia mmoja kutokana na kuendesha Kampeni ya mtandao inayofahamika kama WhisperGate.
Mashambulizi hayo yalilenga kufuta Data muhimu katika Kompyuta za Serikali ya Ukraine, kwa lengo la kusimamisha shughuli za kiuchumi na huduma muhimu, taarifa zaidi zilibainisha kuwa Kitengo 29155 kimekuwa kikiendesha mashambulizi haya tangu mwaka 2020, likiwa na lengo la kupeleleza na kuvuruga juhudi za misaada kwa Ukraine.
Hata hivyo Ujerumani ilijiunga na mashirika ya ujasusi ya nchi zaidi ya kumi na mbili za Magharibi, pamoja na Marekani na Ukraine, kuonesha namna Urusi imekuwa ikiendesha ujasusi na uharibifu wa miundombinu kwa muda mrefu.
Mamlaka za Ujerumani pia zimeituhumu Urusi kwa mashambulizi ya mtandao yaliyoilenga serikali ya Ujerumani, Kampuni za Teknolojia, usafirishaji, na anga, lakini pia zikilenga kuiba na kuchapisha Data nyeti.