Shirika la Afya Dunian (WHO) limeonya kuhusu hatari kubwa ya kuongezeka ugonjwa wa homa ya malaria nchini Ethiopia.
Katika ripoti yake ya karibuni kabisa, shirika hilo limesema kuwa, nchi hiyo ya mashariki mwa Afrika imeripoti zaidi ya wagonjwa milioni 5.9 wa homa malaria, ikiwa ni pamoja na vifo 1,023 kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu hadi Septemba 22.
Ripoti hiyo imesema kuwa, hali hiyo inaonesha kuongezeka na kuenea sana ugonjwa wa malaria nchini Ethiopia ikilinganishwa na kesi milioni 4.5 zilizoripotiwa kati ya Januari 1 hadi Disemba 31 mwaka jana (2023).
Kesi nyingi zimeripotiwa katika majimbo ya Oromia, Amhara, Kusini-Magharibi, Ethiopia Kusini na Benishangul-Gumuz, huku asilimia 50 ya kesi za ugonjwa huo zikiwa zimeripotia huko Oromia ambalo ndilo jimbo kubwa zaidi la Ethiopia.
Ripoti ya WHO imeongeza kuwa, tangu mwaka 2018, idadi ya kesi za homa ya malaria zimekuwa zikiongezeka kila mwaka nchini Ethiopia.
Shirika hilo la Afya Duniani pia limesema kuwa, mashirika ya misaada ya kibindami yanaendelea kuisaidia serikali ya Ethiopia kwa hali mbalimbali ikiwa ni pamoja na vifaa vya kuokoa maisha ya wagonjwa wa malaria hata kwenye maeneo ambayo hayafikiki kiurahisi.
Maeneo yaliyoenea zaidi malaria nchini Ethiopia ni yale ya mabondeni ambayo yanachukua robo tatu ya ardhi ya nchi hiyo.