September 5 2014 kumetokea ajali kubwa za mabasi mawili ya abiria hapa Musoma na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 30 likiwa ni tukio baya lililochukua maisha ya ndugu zetu kwenye tarehe iliyokua imepangwa kufanyika tamasha la Serengeti Fiesta.
Muda mfupi baada ya ajali hiyo, Ruge Mutahaba kutoka kwenye kamati ya maandalizi ya Fiesta alikusanyika na Wasanii wote waliokua waimbe kwenye tamasha hili na kuzungumza na Waandishi wa habari juu ya maamuzi yao waliyofikia kuahirisha tamasha hili kutokana na huu msiba.
‘Isingiwezekana sisi kuendelea na tamasha wakati ndugu zetu wamepoteza maisha, kiukweli huu msiba umenigusa sana’ alisema Shilole, Christian Bella alisema ‘kauli mbiu ya Fiesta mwaka huu ni Sambaza upendo, kwa kuizingatia tumeona ni muhimu tuahirishe kulifanya hili tamasha siku hii manake huu msiba umemgusa kila mmoja…. najua uchungu wa kumpoteza ndugu kwenye kifo cha ghafla kama ajali’
Hii picha hapa juu ni muda mfupi baada ya kuahirishwa kwa fiesta, Wasanii walionyesha moyo mkubwa na kuuweka umaarufu pembeni kisha kuongozana wote kwenda kutembelea Majeruhi hospitali na pia kuwapa misaada mbalimbali waliofiwa na wenye ndugu majeruhi.
Kiukweli Wasanii waliguswa sana na huu msiba ambapo wakiwa hospitalini mmoja alianzisha wazo la kurudi tena leo kujulia hali majeruhi na kutoa misaada mingine kitu ambacho kiliungwa mkono na wengine wote.