Mwanamke mmoja huko Urusi amefariki dunia baada ya kutumia simu aina ya Iphone akiwa bafuni kwake wakati akiwa anaoga huku akiwa anapekua ukurasa wake wa mtandao wa kijamii.
Kwa mujibu wa jirani wa mwanamke huyo, Evgenia Svidirenko mwenye umri wa miaka 24 alikuwa akitazama ukurasa wake wa mtandao wa kijamii kama Facebook lakini kwa taifa la urusi unaoitwa VKontante kabla ya kifo chake kutokea.
Jirani huyo ambaye walikuwa wkaiishi na marehemu Evgenia kwenye jengo moja anayeitwa Yaroslav Dubinina mwenye umri wa miaka 23, aliona mwanadada huyo amechelewa kutoka bafuni baada ya kukaa huko kwa muda mrefu na baada ya kwenda kumtazama alimkuta akiwa anaelea kwenye kibeseni cha kuogea huku akiwa tayari amefariki dunia.
Mwanadada huyo aliyeshuhudia tukio hilo anasema kuwa kitu cha kwanza alichoona ni simu yake aina ya Iphone ambayo ilikuwa kwenye chaja ya simu ambayo ilikuwa chini ya beseni la kuogea ambapo marehemu alikuwemo ndani yake.
Jirani huyo alisema kuwa wakati alipoukuta mwili wa Evgenia ulikuwa bado unatetemeka kutokana na shoti ya umeme ambayo ilianzia kwenye chaja ya simu.
Polisi nchini Urusi bado wanafanya uchunguzi kutambua kwanini chaja hiyo haikukata umeme wakati ilipopata shoti na pia wanaifuatilia simu ya marehemu kuweza kutambua kama ni bidhaa iliyosajiliwa toka kampuni ya Apple.
Kifo cha Evgenia kinakuja siku chache tu baada ya tukio lingine la kifo cha binti mdogo wa umri wa miaka 16 ambaye alifariki dunia kwa mtindo huu huu akiwa anachaji simu yake akiwa bafuni ambapo alipigwa na shoti ya umeme wakati akiwa anaoga.
Mwezi Agosti mwaka jana mamlaka nchini China ziliripoti tukio kama hili baada ya kijana mdogo wa umri kati ya miaka 11 na 17 alipopigwa shoti ya umeme wakati simu yake aina ya iPhone ilipokuwa imechomekwa kwenye chaja isiyo rasmi.
Kijana huyo Wu Weiyan alikutwa na dada yake akiwa amefariki dunia baada ya dada huyo kusikia harufu ya kitu kikungua na alipokwenda kutazama alikuta ndugu yake akiwa amefariki dunia .
Kampuni ya Apple hapo awali imewahi kuonya juu ya hatari za matumizi ya chaja zisizo rasmi ambazo hazijatolewa na wauzaji rasmi wa bidhaa za Apple.