Mauaji yanayotokana na migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji mkoani Morogoro, yanazidi kutikisa baada ya watu wengine watatu kuuawa kwenye Kijiji cha Mbiligi, Kata ya Magole wilayani Kilosa.
Tukio hilo, ambalo limetokea mwezi mmoja tu baada ya mkulima mmoja kuuawa kwenye Bonde la Mgongola wilayani humo, ni kati ya matukio mengi ya mapigano baina ya jamii hizo mbili na ambayo yalijadiliwa kwa kina kwenye mkutano uliopita wa Bunge la Muungano.
Habari kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa, juzi saa 2.00 asubuhi wakulima wapatao 15 walikwenda eneo la Matembele na Ming’oni, jirani na Kijiji cha Mbigili ili kupanda mpunga, lakini saa nne baadaye vijana wawili wa Kimasai walifika na kuhoji sababu za kutumia eneo hilo kwa kilimo wakati ni mali ya Kijiji cha Mabwegela na kuwaamuru waondoke.
Lakini wakulima hao walikaidi na ndipo muda mfupi baadaye likaibuka kundi la wafugaji wapatao 50 na kurejea swali hilo.
Kwa mujibu wa habari hizo, wakulima waliamua kutoroka, ndipo baadhi yao waliposhambuliwa kwa mikuki, virungu, mishale na visu na kusababisha vifo vya watu hao watatu.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Elias Tarimo alisema watu wengine kadhaa walijeruhiwa na wamelazwa katika Kituo cha Afya cha St Joseph cha Dumila, Kilosa.
MWANANCHI
Wakala wa Ukaguzi wa Madini nchini (TMAA) umetangaza dau nono kwa yeyote atakayewezesha kukamatwa kwa mfanyabiashara yeyote anayesafirisha madini kwa njia za magendo kupitia njia za panya zaidi ya 400 zilizopo nchini.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TMAA, Bruno Mteta alipokuwa akitoa taarifa ya mwaka uliopita ya mapambano dhidi ya magendo ya madini mbele ya waandishi wa habari.
“Kwa kipindi cha kuanzia Januari mpaka Desemba mwaka jana, wakala umeweza kukamata watoroshaji wa madini ya aina mbalimbali katika matukio 27 tofauti. Tunawaomba Watanzania wazalendo kushirikiana nasi ili kuwabaini watu wote wanaojishughulisha na magendo haya na tayari wizara imethibitisha zawadi ya asilimia tano ya thamani ya madini yatakayokamatwa itatolewa,”:- Mteta.
Wakala umeanza utekelezaji wa mkakati huo ulioratibiwa tangu mwaka 2012 wakati huo Serikali ilisema itatoa asilimia 30 ya thamani ya mzigo baada ya kugundua kuwapo kwa watu wanaolipwa asilimia 10 kusaidia kufanikisha magendo hayo na hivyo kuchangia kuikosesha mapato.
Alisema hilo lilikuwa ni pendekezo linaloendelea kutekelezwa na kwamba, kiasi hicho ni haki ya mtoa taarifa ambaye hatotajwa mahali popote katika mchakato mzima wa hatua za kisheria.
“Utoroshaji wa madini umekithiri, zinahitajika nguvu za pamoja ili kuhakikisha Taifa linanufaika na rasilimali zake. Atakayekamatwa mali yake itataifishwa na kama ni kampuni basi itanyang’anywa leseni yake na kutoruhusiwa tena kufanya shughuli zake hapa nchini,” :- Mteta.
Kwa madini yanayoingizwa ili yasafirishwe nje bila kuwa na vibali, alisema nayo yakikamatwa yatataifishwa hivyo kuwataka wote wanaofanya hivyo kutumia ofisi za ukaguzi zilizoko mipakani kuhalalisha madini waliyonayo.
NIPASHE
Siku tatu baada ya mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (albino), Yohana Bahati mwenye umri wa mwaka mmoja, kutekwa na watu wasiofahamika, hatimaye mwili wake umepatikana ukiwa umekatwa miguu, mikono yote na kiwiliwili chake kufukiwa shambani katika Kitongoji cha Mapinduzi, Kijiji cha Rumasa ndani ya hifadhi ya msitu wa Biharamulo Wilaya ya Chato, mkoani Geita.
Mtoto huyo alinyakuliwa Jumapili iliyopita nyumbani kwao saa 2:15 usiku akiwa amebebwa na mama yake mzazi, Esther Jonathan (30), baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa mapanga usoni, mwili wake ulipatikana baada ya msako uliofanywa na wananchi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo, alisema mwili huo ulipatikana juzi saa 12:30 jioni katika shamba la mahindi lisilo rasmi kutokana na kulimwa ndani ya hifadhi ya msitu wa Biharamulo, wilayani Chato.
Mwili huo ulipatikana kutokana na jitihada za wananchi walioshirikiana na makachero wa Jeshi la Polisi baada ya mwananchi mmoja (jina wanalo polisi) kuonekana akikatisha katika msitu huo, huku upande wa shati lake ukionekana ukiwa na damu.
Kamanda Konyo alisema baada ya raia huyo kuona viashiria hivyo, alilazimika kutoa taarifa kwa wananchi wenzake, ambao walifuatilia mwelekeo wa nguo hiyo na kufanikiwa kuona shimo limefunikwa na udongo mbichi kisha walipofanikiwa kufukua wakauona mwili huo.
“Baada ya wananchi hao kufukua shimo hilo, walifanikiwa kukuta mwili wa mtoto Yohana ukiwa umekatwa mikono na miguu yote…baadaye mwili huo ulichukuliwa na askari hadi katika Hospitali ya Wilaya ya Chato kwa ajili ya uchunguzi zaidi,”:- Konyo.
Hata hivyo, baada ya kuupata mwili huo, wananchi hao walipandwa na jazba na kumtuhumu mwananchi huyo kuhusika na mauaji hayo na kuanza kumshambulia kabla ya polisi kuingilia kati na kumuokoa kutoka mazingira hayo.
NIPASHE
Wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) jijini Dar es Salaam wametangaza azma yao ya kumuunga mkono Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa (pichani), iwapo ataamua kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Wamesema wataanza kutekeleza azma yao hiyo kwa vitendo kwa kumsindikiza atakapokwenda kuchukua fomu za kukiomba ridhaa chama chake ya kuwania nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Kauli hiyo ilitolewa na Mbunge wa Bunge la Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho, Hafsa Masumai, kwa niaba ya wenzake, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam juzi.
Alisema wanamuunga mkono Lowassa kwa kuwa ni miongoni mwa viongozi watetezi wa masuala ya elimu.
“Wanafunzi wamekuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa sugu hata kutatuliwa na serikali, ikiwamo mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu,” :-Masumai.
Aliongeza: “Tutamuunga mkono Lowassa, kwani ni kiongozi, ambaye anaonekana kujali elimu na tunaamini anaweza kutatua matatizo haya, ambayo yamekuwa yanatukabili kwa muda mrefu.”
Alisema Lowassa mbali na kuwa kiongozi aliyetetea elimu pia amekuwa akisaidia vijana katika nyanja mbalimbali, ikiwamo kuwasaidia kwenye vikundi vyao na kujikwamua dhidi ya makali ya maisha.
NIPASHE
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, amemkosoa Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM) Andrew Chenge, kwa kujiita ‘nyoka wa makengeza’ kwa madai kwamba, anastahili kuitwa ‘nyoka wa ufisadi’.
Mnyika katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, alisema wananchi wanapaswa kumuita Chenge ‘nyoka wa ufisadi’ badala ya kujisifia kuwa ni ‘nyoka mwenye makengeza’ kwa kuwa amehusika katika kutafuna mali ya umma.
“Kauli ya Chenge kama ilivyokuwa kwa ile ya ‘vijisenti’, ni kiburi cha kifisadi,”:- Mnyika.
Chenge alitoa kauli hiyo juzi wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mahaha kata ya Vunamala, wilayani Bariadi, mkoani Simiyu, akiwaeleza wananchi wa jimbo lake kuwa aitwe nyoka kwa kuwa ni mjanja wa kutafuta fedha kwa ajili ya wananchi wake.
Mnyika alisema udhaifu wa serikali na vyombo vyenye mamlaka ya kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya tuhuma za ufisadi unaodaiwa kufanywa na Chenge na watuhumiwa wengine wa ufisadi ndiyo unaowalinda nyoka wa ufisadi na sasa wanajigamba kuwa ni wajanja wa kutafuta fedha kifisadi.
“Chenge anadai kwamba yeye ni mjanja wa kutafuta fedha za wananchi wa jimbo lake ili hali yeye na wenzake wamesababisha wananchi wa jimbo lake na mengine nchini kukosa fedha nyingi zaidi za miradi ya maendeleo mpaka hivi sasa kutokana na ufisadi wa Tegeta-Escrow,” Mnyika.
NIPASHE
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Shamariwa ‘A’, Kata ya Igoma, Wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza, Julias Makoye (CCM), amekutwa amejinyonga juu ya mti ulio jirani na nyumba yake usiku wa jana.
Makoye aliyetangazwa mshindi wa kiti hicho katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Desemba 14, mwaka jana, ameuongoza mtaa huo kwa awamu ya pili baada ya kuongoza miaka mitano iliyopita.
Mke wa marehemu, Ivona Polikalapo, alisema saa 10 juzi jioni alimsikia mumewe akiongea na mtu kwenye simu yake ya mkononi na kumsisitiza anahitaji mzigo wake wote.
“Jana (juzi) saa 10 jioni nilimsikia mume wangu akiongea na mtu katika simu na kutaka alipwe mzigo wake wote kutokana na kukaa muda mrefu, lakini aliyekuwa akizungumza naye sikumfahamu ni nani,”:- Polikalapo.
Aidha, alisema ilipofika saa 10 alfajiri ya jana, mbwa wao walisikika wakibweka kwa muda mrefu hali iliyomfanya marehemu atoke nje kuangalia kilichopo katika banda lao la mifugo huku (mke) akiendelea kuandaa chakula cha mifugo hao.
“Baada ya mume wangu kuamka na kwenda kuangalia kilichopo nje, hakuweza kurejea ndani hadi pale nilipotoka kwenda kumwaga uchafu shimoni nikashangaa baada ya kumuona ananing’inia juu ya mti…nilipojaribu kumuita hakuitika,” alisema.
Hata hivyo, mama huyo anasema haamini kama mume wake amejinyonga bali kanyongwa kutokana na mti aliojitundika kutoonekana kuwapo na jiwe la ‘sapoti’ ili kutekeleza azma yake hiyo.
MTANZANIA
Raia wa kigeni wanaofanya biashara haramu ya madini wamekamatwa na madini yenye thamani ya Dola za Marekani 113,807.11 sawa Sh milioni 641.853 katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TMAA, Bron Mteta alisema watu hao walikamatwa katika matukio 27 tofauti huku wakiwa na madini ya aina mbalimbali.
Alisema miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na lile la Juni 12 mwaka jana ambapo raia mmoja alikamatwa kwenye uwanja huo akiwa na madini ya vito vyenye uzito wa gramu 1,290 yenye thamani ya dola za Marekani 11,591.82.
Alisema mtuhumiwa alifikishwa mahakamani na kuhukumiwa adhabu ya kulipa faini ya Sh 300,000.
Alisema katika tukio jingine la Desemba 14 mwaka jana,raia mwingine wa kigeni alikamatwa kwenye uwanja huo akiwa na madini ya vito ya uzito wa karati 288 na thamani ya dola za Kimarekani 23,235.50.
Alisema mpaka sasa hatua za kisheria zimechukuliwa kwa mtuhumiwa huyo ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani na kupewa adhabu ya kulipa faini ya sh.500,000.
HABARILEO
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) imeshikwa kigugumizi kuhusu suala la kushusha nauli ya magari ya abiria kwa kutoa sababu za kisheria pamoja na ukokotoaji wa tozo.
Kwa mujibu wa Kanuni za Tozo pamoja na Sheria, Sumatra inapaswa kurejea tozo ya huduma baada ya mtoa huduma au mtumiaji wa huduma kupitia Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na Sumatra (Sumatra CCC) kuwasilisha maombi.
Pia huridhia viwango kwa kuzingatia masuala yote yanayoathiri gharama za uendeshaji, mafuta ikiwa ni moja ya eneo muhimu katika kukokotoa tozo zinazostahili kuridhiwa.
Meneja Mawasiliano kwa Umma, David Mziray alisema mwasilishaji wa maombi awe ni mtoa huduma au Sumatra CCC anapaswa atoe maelezo ya kina kuhusu sababu za kuomba mabadiliko ya tozo, jinsi alivyoathirika, ikiwa ni pamoja na kuambatisha nyaraka muhimu zinazoweza kuthibitisha hoja zake.
Alisema maoni ya wadau huzingatiwa kwa pamoja na masuala yaliyoainishwa katika Sheria ya Sumatra ambayo inatoa muongozo wa masuala ya kuzingatia katika kuridhia viwango vya tozo mbalimbali.
Alisema masuala hayo ni pamoja na gharama za uendeshaji, haja ya kukuza ushindani katika soko na kulinda maslahi ya watumia huduma na watoa huduma.
Akizungumzia kuridhia viwango kwa kuzingatia masuala yote yanayoathiri gharama za uendeshaji wanazingatia umuhimu wa kuwa na huduma endelevu, kulinda maslahi ya watumiaji na watoa huduma kwa kuweka mizania sawa na gharama za uendeshaji ikiwa ni pamoja na mishahara na gharama za matengenezo.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram, na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook