Safari ya mwisho ya mbunge wa Mbinga Magharibi John Damiano Komba jana ilihitimishwa saa 9.25 alasiri wakati mwili wake ulipofunikwa na mfuniko mkubwa wa zege uliobebwa na gari maarufu kwa jina la “kijiko”.
Haikuwa kitu cha kawaida wakati gari hilo kubwa likishusha mfuniko huo wa zege kwenye kaburi la mwimbaji huyo maarufu wa nyimbo za uhamasishaji za CCM na kiongozi wa kundi la Tanzania One Theatre (TOT), lakini majonzi yaliwafanya waombolezaji kulichukulia tukio hilo kuwa la kawaida.
Safari ya Komba, iliyoanza miaka 61 iliyopita kwenye kijiji cha Lituhi ambako aliazikwa jana, ilikamilishwa kwa salamu mbalimbali ambazo zilielezea ushupavu wa kapteni huyo mstaafu wa jeshi.
Mazishi hayo yaliyohudhuriwa na mamia ya wananchi, wakiwamo viongozi mbalimbaliwakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete na mkewe Salma, yalifanyika katika makaburi ya Misheni,katika Kijiji cha Lituhi (Bundi) wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.
Nyuso za majonzi zilitawala kwa waombolezaji waliojitokeza nyumbani kwa marehemu, takriban mita 500 kutoka katika makaburi hayo na baadaye katika misa iliyofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Lituhi, ikiongozwa na Askofu John Ndimbo wa Jimbo Katoliki la Mbinga.
Kaimu katibu wa Bunge, John Joel, akisoma wasifu wa marehemu, alisema Kapteni Komba aliyefariki dunia Februari 28, mwaka huu akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam, alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya shinikizo la damu na mara kadhaa Ofisi ya Bunge ilimpeleka India kwa matibabu.
Mazishi hayo yalishuhudiwa na viongozi mbalimbali, akiwamo Edward Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Utaratibu na Bunge), Jenister Mhagama na mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi.
Wengine ni Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi, Ali Abdallah Ali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Prof. Mark Mwandosya na Spika wa Bunge, Anne Makinda.
MWANANCHI
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imepunguza bei ya mafuta kwa mara nyingine katika kipindi cha miezi mitatu huku punguzo la sasa likitajwa kuwa ni la chini zaidi katika kipindi cha miaka sita.
Punguzo la chini zaidi la mafuta liliwahi kutokea mwaka 2009 ambapo bei ya Petroli ilishuka kutoka Sh2,200 hadi Sh1,147.
Jana Ewura ilitangaza kushuka kwa bei za mafuta ambayo kuanzia leo petrol itauzwa Sh1,652, dizeli Sh1,563 na mafuta ya taa yatauzwa kwa Sh1,523 kwa Dar es Salaam.
Hata hivyo, mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo jana aliiambia Mwananchi kuwa kushuka huko kwa bei ya mafuta si kwa kutisha kwani ni kawaida kwa nishati hiyo kupanda na kushuka kwa kasi.
“Hii ni mara ya pili kwa bei ya mafuta kushuka kwa kiasi hiki hadi kufikia Sh1,652. Iliwahi kutokea Mei mwaka 2009, na ikapanda tena kwa kasi hadi kufikia Sh2,000 na zaidi. Baada ya hapo haikuwahi kushuka,” alisema. Hata hivyo, Kaguo alisema kwa kipindi kile viwango vya kubadilisha fedha vilikuwa ni tofauti, akitoa mfano wa mwaka 2009 kuwa Dola moja ilikuwa chini ya Sh1,000 lakini kwa sasa ni zaidi ya Sh1,800.”
MWANANCHI
Wakazi wa jijini hapa jana walizua tafrani baada ya kufunga ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa muda wakidai kupewa majibu kuhusu tatizo la upatikanaji wa umeme lililodumu kwa zaidi ya siku tano.
Tukio hilo lilitokea jana saa 4:00 asubuhi baada ya wateja hao kusubiri majibu kutoka kwa wahusika, ambao awali walitangaziwa kuwa huduma hiyo ingeanza kupatikana juzi, lakini mpaka jana tatizo hilo lilikuwa likiendelea.
Wakazi hao waliwafungia wafanyakazi wa Tanesco wa kitengo cha malipo, wakisema kuwa hawafanyi kazi yoyote na hivyo hawatakiwi kutoka nje. Hali hiyo ilidumu hadi askari wa walipowasili na kuwashauri waondoke.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti ofisini hapo, wateja hao walisema baada ya kukosekana kwa huduma ya luku kwa siku tatu, jana kupitia simu zao za mkononi walipokea ujumbe uliowataarifu kuwa huduma hiyo ingeanza kutolewa jana kwa mawakala na katika ofisi za Tanesco, hata hivyo hali haikuwa hivyo.
Mkazi wa Mwanjelwa, Dickson Mwangunga alisema watendaji wa shirika hilo wanatoa taarifa zisizo sahihi na kusababisha usumbufu.
“Ni vema kama wangetoa taarifa sahihi, watu tumefika hapa kwa ajili ya kununua umeme, lakini huduma hiyo haipo. Baadhi yao wanatuambia eti hali bado haijatengemaa, wengine wanasema tusubiri na muda unazidi kwenda, sasa nani mkweli? ndiyo maana tumeamua kuzifunga ofisi zao watupe jibu sahihi lini huduma hii itatengemaa,”:- Mwangunga.
Hata hivyo, sakata hilo liliokolewa na mkuu wa upelelezi wa Wilaya ya Mbeya, Kitinkwi Mtatiro ambaye alifika katika ofisi hizo na kuwaomba wateja hao warejee nyumbani hadi watakapopewa taarifa ya kurejeshwa kwa huduma na uongozi wa Tanesco.
“Nawaomba mfungue milango ya ofisi, waacheni wafanye kazi hili ni tatizo limetokea. Hata wao hawapendi karaha hii itokee ni vema mkawa watulivu msipende kujichukulia sheria mkononi. Jambo hili linaweza kuvuruga amani,” :- Mtatiro.
Akizungumzia hali hiyo, meneja wa Tanesco wa Mbeya, Amos Maganga aliwaomba wananchi kuwa watulivu kwa kuwa tatizo hilo ni la kitaifa na mara mitambo itakaporekebishwa watajulishwa kupitia simu zao za mkononi.
Jijini Dar es Salaam, wananchi waliendelea kulia na tatizo hilo lililodumu kwa siku tatu mfululizo.
Baadhi yao wamelalamikia hasara wanayoipata kwa sababu ya kukosa umeme na kushindwa kufanya kazi za uzalishaji zinazotegemea uwapo wa umeme.
MWANANCHI
Mfanyabiashara maarufu nchini na Mbunge wa Singida Mjini (CCM), Mohammed Dewji kwa mara ya kwanza ameingia kwenye orodha ya mabilionea 29, akiwa tajiri kijana kuliko wote barani Afrika.
Jarida la Forbes la Marekani limemtaja Dewji (39), katika nafasi ya 24 ya matajiri wa Afrika akiwa na utajiri wa Dola 1.3 bilioni za Marekani (Sh2.34 trilioni) unaotokana na biashara mbalimbali anazozifanya kupitia kampuni yake ya Mohammed Enterprises (Metl Group).
“Dewji alibadilisha biashara aliyoanzisha baba yake kutoka uuzaji bidhaa na kuwa na viwanda vya Metl,” inasema sehemu ya habari inayomuhusu bilionea huyo Mtanzania iliyochapishwa juzi jioni.
“Alinunua viwanda vya nguo na mafuta vilivyokuwa vinamilikiwa na Serikali kwa bei ndogo na kuvifanya viwe na faida zaidi kwa kutumia mtindo wa kisasa wa menejimenti,” inaongeza ripoti hiyo.
Metl ina viwanda vya kutengeneza nguo na bidhaa nyingine za matumizi ya binadamu vikiwamo vyakula, sabuni na vinywaji. Pia ina mapato yanayozidi Dola 1.4 milioni za Marekani (Sh2.5 trilioni) kwa mwaka.
Katika kampuni hiyo, ambayo imekuwa na ushindani dhidi ya kampuni kubwa nyingine kama Said Salim Bakhresa, Dewji anamiliki asilimia 75 ya hisa zote.
Dewji anashika nafasi mbili juu zaidi ya kada maarufu wa CCM na aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Igunga, Aziz Rostam (50) aliyewekwa nafasi ya mwisho.
Rostam amefungana nafasi ya 26 na mabilionea wa Nigeria, Abdulsamad Rabiu na Femi Otedola wenye utajiri wa Sh1.8 trilioni kila mmoja.
Orodha hiyo ya 29 bora inaoongozwa na bilionea wa Nigeria, Aliko Dangote akiwa na utajiri wa Dola 15.7 bilioni za Marekani (Sh28.2 trilioni), kiwango ambacho ni mara moja na nusu ya bajeti ya Serikali ya Tanzania ya mwaka 2014/15.
NIPASHE
Watu wanane wameuawa akiwamo mke na mume wake kutokana na imani za kishirikina katika mikoa ya Mara na Dodoma.
Watu hao wameuawa wakituhumiwa kuzuia mvua isinyeshe na kusababisha vijiji vyao kukabiliwa na tatizo la ukame.
Katika tukio la kwanza, watu watano waliuawa katika kijiji cha Park Nyigoti wilayani Serengeti mkoa wa Mara usiku wa kuamkia jana.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ernest Kimola, alisema watu hao ambao hata hivyo hakuwataja majina waliuawa na wanakijiji wenzao wakiwatuhumu kuzuia mvua isinyeshe, hivyo kusababisha ukame kijijini hapo.
Kimola alisema juzi wakazi wa kijiji hicho waliitisha mkutano na kuanza kutafakari sababu za kijiji chao kukumbwa na ukame uliosababisha mito na mashamba ya mimea yaliyolimwa msimu huu kuanza kukauka na kuelezana kuwa hali hiyo imetokana na ushirikina unaofanywa na baadhi ya wenzao.
Alisema kufuatia hali hiyo walianza kuwataja kwa majina watuhumiwa hao na hivyo siku iliyofuata asubuhi walianza kuvamiwa nyumba zao na kuwashambulia kwa kipigo na kuwaua.
“Wananchi waliwachomoa katika nyumba zao watuhumiwa hao na kuanza kuwashambulia kwa silaha za jadi hadi kuwaua,” alisema.
Kimola alisema Jeshi la Polisi limeendesha msako mkali na kuwakamata watu sita kwa tuhuma za mauaji hayo huku likiwasaka wengine.
NIPASHE
Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja, jana alipanda ‘kizimbani’ mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kujibu malalamiko dhidi yake ya kupokea zaidi ya Sh. milioni 40.4 kutoka kwa mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd, James Rugemalira, kinyume cha sheria ya maadili na kuliomba baraza hilo kwamba, iwapo litatumia rungu lake kutoa mwongozo wa adhabu, lisianzie kwake, kwani kitendo alichokifanya hufanywa pia na wabunge wengine.
Ngeleja (47), ambaye amewahi pia kuwa naibu waziri na Waziri wa Nishati na Madini, alisema hayo wakati akihitimisha utetezi wake baada ya kusomewa malalamiko hayo dhidi yake na wanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma mbele ya baraza hilo, linaloongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Hamisi Msumi, jijini Dar es Salaam jana.
“Naomba baraza lako litoe mwongozo utakaokuwa una unafuu kwangu, sababu sikutenda hili kwa nia mbaya, bali ni kwa utaratibu ambao unatumika Tanzania. Mimi ni Mtanzania, mzalendo, mwaminifu kama walivyo wengine,” alisema Ngeleja kwa upole na kwa unyenyekevu wa hali ya juu akiwa amesimama ‘kizimbani’ mbele ya baraza hilo jana.
Aliongeza: “Baraza lako litoe mwongozo. Rungu la mwongozo wako lisianzie kwangu, sababu imethibitika wabunge wengine wamehusika…sikuwahi kupotoka kwenda kinyume cha maadili ya utumishi. Baraza lako litafakari kabla ya kutoa maamuzi.”
Ngeleja alifikia kutamka hayo baada ya Mwanasheria wa Baraza hilo, Getrude Cyriacus, kuhitimisha hoja za malalamiko hayo akiliomba baraza lione umuhimu wa kupendekeza kwa mamlaka husika adhabu kali dhidi ya Ngeleja ili liwe fundisho kwa watumishi wengine wa umma.
Ngeleja alikiri kupokea fedha hizo kutoka kwa Rugemalira, lakini alisema hazikutolewa kwake kama fadhila za kiuchumi kama malalamiko yaliyowasilishwa dhidi yake katika baraza hilo jana yanavyoeleza.
Alidai fedha hizo aliomba na kupewa zikiwa ni msaada, ambao hautofautiani na misaada inayopokelewa na wabunge wengine, ambayo hubarikiwa na Bunge.
Ngeleja alidai mmoja wa wabunge walionufaika na misaada ya fedha za wafadhili, ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ambaye kisheria ni mtumishi wa umma.
Alidai Zitto alinufaika na msaada wa zaidi ya Sh. milioni 30 na dola za Marekani 5,000 kutoka kwa Kampuni ya Pan Africa Power (PAP) na Independent Power Tanzania Limited (IPTL) alizopata kwa matumizi yake binafsi.
MTANZANIA
Tanzania kwa kushirikiana na Uturuki inatarajia kujenga kituo kikubwa cha albino ambacho kitakuwa na huduma mbalimbali muhimu ikiwamo shule na afya.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema kituo hicho kitawasaidia albino kupata huduma muhimu wakiwa kwenye mikono salama.
Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana baada ya kumalizika kikao cha ndani cha mabalozi na wawakilishi wa nchi mbalimbali.
“Rais Jakaya Kikwete alizungumza na Serikali ya Uturuki kuangalia jinsi tunavyoweza kuwasaidia wenzetu wenye ulemavu wa ngozi.
“Miongoni mwa makubaliano hayo ni kujenga kituo kikubwa cha walemavu hao ambacho kitakuwa na huduma mbalimbali ambazo ni pamoja na shule, kituo cha afya ambacho kitakuwa kinatoa huduma za matibabu kwa walemavu hao,”alisema.
Membe alisema kituo hicho kitakuwa na watalaam wa kutoa mafunzo mbalimbali pamoja na ulinzi ikiwa ni mkakati wa serikali kuhakikisha tatizo la mauaji ya albino linakwisha nchini.
HABARILEO
Pacha walioungana kiwiliwili, Consolata na Maria Mwakikuti (18) wa Kijiji cha Ikonda wilayani Makete mkoani Njombe wamefaulu mtihani wao wa kuhitimu kidato cha nne kwa alama sawa isipokuwa masomo mawili.
Ufaulu wao wa alama ya credit 2.0, huku wakiwa wamefanya vizuri katika Kiingereza na Baiolojia, umekuja wakati wanafunzi wengi wa shule ya Sekondari Maria Consolata iliyoko mkoani Njombe, wakiwa wamefanya vibaya katika matokeo ya mwaka jana.
Kutokana na alama walizopata, zinawawezesha Maria na Consolata kuendelea na masomo ya Kidato cha Tano, Julai mwaka huu. Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, wasichana hao walioko kijijini kwao Ikonda , walisema masomo waliyotofautiana katika ufaulu ni Kemia ambalo Maria amepata C na Consolata D na Kiingereza ambalo Maria amepata B na Consolata B+. Katika matokeo hayo ambayo kila mmoja alikuwa na namba yake ya mtihani (MariaS. 283/0004 na Consotala S 283/0009), masomo ambayo wamelingana ni Uraia wakiwa na E, Historia C, Jiografia E, Kiswahili C, Baolojia B na Hesabu C.
“Tumefurahia sana kufaulu, tutaendelea na masomo ya kidato cha tano na sita shule hapo Julai,tutasoma mchepuo wa CBG (Kemia,Biolojia na Jiografia) au HGL, (Historia,Jiografia na Kiingereza),”:- Consolata.
Aliendelea kusema, “tunategemea kwenda Shule ya Sekondari ya Udzungwa iko karibu na shule tuliyosoma kidato cha kwanza hadi cha nne ya Maria Consolata kule Kidabaga, Kilolo.” Kwa upande wake Maria, alisema amefurahi na matumaini yao ni kujitahidi kusoma kwa bidii zaidi wafaulu na kujiunga na elimu ya juu.
“Nimefurahi mimi na Consolata, tulipigiwa simu na walimu wakatuambia matokeo yetu, mama yetu mlezi amefurahi na Mungu akipenda tutaanza masomo mwezi Julai; Ya kidato cha tano”,alisema Maria ambaye kwa mujibu wake, wana ndoto za kuwa wahasibu.
Alisema kwa sasa wako likizo wamepumzika nyumbani kwao Ikonda chini ya uangalizi wa mama yao mlezi na dada yao msaidizi, Magdalena Mbilinyi .Wanatarajia kurudi Kilolo, kwenye Kituo cha Nyota ya Asubuhi.
JAMBOLEO
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya mwelekeo wa mvua za masika katika kipindi cha Machi mpaka Mei na kusema kuwa hali ya mvua haitarajiwi kuwa ya kuridhisha katika maeneo mengi ya nchi.
TMA imesema kuwa kutokana na kuwapo kwa kiwango hicho cha mvua, maeneo mengi yatakumbwa na ukame.
Hayo yalisemwa jana na mkurugenzi mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alipokuwa akitoa mwelekeo wa hali ya hewa katika maeneo mengi ya nchi ambayo hayajapata mvua za masika za kutosha.
Aliitaja mikoa inayotarajiwa kupata mvua za wastani mpaka chini ya wastani kuwa ni Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Unguja na Pemba, Morogoro, Kilimanjaro, Arusha na Simiyu.
Mikoa mingine ni Singida, Dodoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Kigoma, Shinyanga na Manyara ambayo pia inatarajiwa kupata kiasi kidogo cha mvua.
Dk Kijazi alisema Kanda ya Ziwa inayohusisha mikoa ya Mwanza, Geita, Mara na Kagera inatarajiwa kupata mvua za wastani mpaka juu ya wastani.
Akizungumzia utabiri huo katika sekta ya kilimo, Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula, Karim Mtambo aliwataka wakulima wanaoishi katika maeneo yatakayopata mvua chini ya wastani kulima mazao yanayokomaa haraka na kustahamili ukame.
“Mikoa ya kanda ya Ziwa Victoria inaweza kupata mvua za wastani mpaka juu ya wastani, hivyo mamlaka husika zinapaswa kujiandaa kwa hali yoyote inayoweza kujitokeza,”- Dk Kijazi.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook