Miamba wa soka barani Afrika, Al-Ahly ya Misri wameipiku timu ya AC Milan ya Italia, timu ambayo inatambuliwa kutwaa makombe mengi kimataifa.
Mabingwa hao watetezi wa ligi kuu ya mabingwa barani Afrika, wameweza kuipiku AC Milan kufuatia ushindi wao dhidi ya CS Sfaxienya Tunisia pale ilipowachabanga magoli 3-2 Alhamisi iliyopita mjini Cairo na kutwaa ubingwa wa CAF Super Cup, wakifikisha mataji 19, moja zaidi ya mataji 18 ya AC Milan.
Al-Ahly imeshinda mara 8 kombe la mabingwa barani Afrika, mwaka 1982,1987,2001,2005,2006, 2008, 2012, na 2013.
Makombe 4 ni ubingwa wa Kombe la washindi 1984,1985,1986, 1993.
Mara sita imetwaa kombe la CAF Super Cup 2002, 2006,2007,2009, 2013, na 2014 na mmoja likiwa la Afro-Asian Cup mwaka 1988.
AC Milan ya Italia imetwaa makombe 18 kimataifa. Saba yakiwa ya mabingwa wa UEFA, matano, UEFA Super Cup, mawili ya Kombe la Washindi UEFA, makombe matatu ya kimabara na moja likiwa ni klabu bingwa ya dunia ya FIFA.
Rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika, CAF, Issa Hayatou ameipongeza Ahly kwa mafanikio hayo, akieleza kuwa ni maendeleo makubwa katika soka la Afrika.
Al-Ahly wiki hii itaanza kampeni ya kutetea ubingwa wake kwa vilabu bingwa barani Afrika, itakapomenyana na mabingwa wa Tanzania, Young Africans,maarufu kama YANGA, jijini Dar es Salaam, Jumamosi wiki hii.