Jeshi la Myanmar limetangaza kupunguza miaka sita kutoka kwenye kifungo cha miaka 30 cha Kiongozi wa Nchi hiyo aliyeondolewa madarakani, Aung San Suu Kyi.
Msemaji wa Jeshi Zaw Min Tun, amesema miaka hiyo imeondolewa katika kifungo chake baada ya tangazo kwamba amesamehewa katika kesi tano zinazomkabili lakini bado Kiongozi huyo wa zamani anakabiliwa na kesi 14 licha ya msamaha huo wa Jeshi, kumekuwa na hofu kuhusiana na hali ya kiafya ya Suu Kyi, wiki iliyopita Jeshi lilimhamisha kutoka Jela na kumpeleka katika jengo la Serikali.
Itakumbukwa mwaka 1991, Aung San Suu Kyi alikabidhiwa tuzo ya amani ya Nobel akiwa chini ya kifungo cha nyumbani na alisifiwa kwa kuwa mfano mzuri wa kutetea wanyonge, mwaka 2015 aliongoza Chama chake cha National League for Demoracy NLD kupata ushindi katika uchaguzi wa wazi uliokuwa na ushindani mkali nchini Myanmar katika kipindi cha miaka 25
Aliwahi kuwekwa kizuizini kwa miaka 15 kati ya mwaka 1989 na 2010 ambapo harakati zake za kuleta Demokrasia katika Taifa hilo ambalo limekuwa likitawaliwa kijeshi zilimfanya kuonekana kama nembo ya kimataifa ya upinzani wa amani wakati wa ukandamizaji.
Licha ya ushindi wake mkubwa mwaka 2015 , katiba ya Myanmar ilimzuia yeye kuwa Rais kwasababu ana Watoto ambao ni wa Mataifa ya kigeni.