Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, ametengua nafasi ya Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mkoa wa Pwani na Lindi kutokana na kutoridhishwa na usimamizi na ufuatiliaji wa matumizi ya barabara ya Dar es Salaam – Kilwa – Lindi hadi Mingoyo yenye urefu takriban kilometa 450.
Aidha, ameagiza Mameneja wapya wa mikoa hiyo na mameneja wa mikoa mingine kuhakikisha wanaziba mashimo yote yaliyopo kwenye barabara zao ndani ya saa 48 kuanzia muda wa shimo hilo linapojitokeza.
“Nimetengua nafasi za watendaji hawa wawili kwa makosa yaliyojitokeza katika barabara hizi zinazounganisha mkoa kwa mkoa na hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu nahitaji wananchi wawe wanapita salama katika barabara hii”, Kamwelwe.
“Fedha zipo sasa sitarajii kuona barabara yoyote hapa nchini ina mashimo, huyo Meneja ambaye barabara zake zina mashimo tutamalizana hapo hapo”, Kamwelwe.
“Tunaleta watalaamu katika barabara hii kwa ajili ya kuanza kusanifu upya na kuona kwanini imeharibika kabla ya wakati wake na maandalizi yanaendelea vizuri”, Kamwelwe