Mamlaka ya Udhibiti huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza kushuka kwa bei za mafuta zinazoanza kutumika leo Jumatano Desemba 2, 2020.
Kwa mujibu wa EWURA, bei ya lita moja ya mafuta ya petroli yaliyopokelewa kupitia bandari ya DSM imepungua kwa Sh.37.36, dizeli imepungua lita moja kwa Sh46.81 huku mafuta ya taa yakipungua kwa Sh86.02 kwa lita ikilinganishwa na bei zilizoanzia Novemba 4, 2020.
Hii inamaanisha kwamba mtumiaji wa bidhaa hizo atakuwa na unafuu wa Sh37.36 kwa kila lita ya petroli, Sh46.81 kwa kila lita dizeli na atakayenunua mafuta ya taa atakuwa na unafuu wa Sh86.02 kwa kila lita.
Kwa mujibu wa taarifa ya EWURA iliyotolewa leo Jumanne Desemba mosi, 2020 inabainisha kuwa mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara bei za rejareja za petroli zimepungua kwa Sh107 kwa lita, dizeli Sh27. Bei ya jumla ya petroli imepungua kwa Sh106.40 na dizeli Sh27.28.
“Hata hivyo bei za mafuta ya taa zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo la Novemba 4, 2020,” inaeleza taarifa ya mamlaka hiyo iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi mkuu wake, Godfrey Chibulunje.
Katika Mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma bei za rejareja za petroli zimepungua kwa Sh. 70 kwa lita, dizeli Sh.4 na bei za jumla za petroli zimepungua kwa Sh69.38 kwa lita, dizeli Sh4.32 ikilinganishwa na bei za mwezi uliopita.