Beki wa kulia wa Manchester United Rafael Da Silva yuko mbioni kuihama klabu hii akiwa karibu kabisa na uhamisho kuelekea klabu ya Olympique Marseile ya nchini Ufaransa ambayo amekuwa akifanya nayo mazungumzo kwa muda wa siku kadhaa .
Da Silva anaihama klabu hii takribani miaka miwili baada ya pacha wake Fabio Da Silva naye kuhama akijiunga na timu Cardiff City ya huko Wales inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini England .
Kuondoka kwa Rafael kumekuwa kwenye mpango kwa muda sasa tangu ilipofahamika wazi kuwa Mbrazil huyo hatakuwa kwenye mipango ya muda mrefu ya kocha Louis Van Gaal .
Kocha huyo kwa muda amekuwa akimtumia Antonio Valencia ambaye kwa asili ni winga katika nafasi ya beki wa kulia hata pale ambapo Rafael amekuwa hasumbuliwi na matatizo ya majeraha na kwa msimu huu tayari United imemsajili beki Mtaliano Matteo Darmian jambo linalofanya nafasi ya Rafael kuwa finyu .
Rafael Da Silva amekuwa na United kwa kipindi cha muda wa miaka saba tangu mwaka 2008 alipojiunga rasmi na timu hiyo ambayo ilimsajili yeye na pacha wake tangu wakiwa na miaka 15 na walilazimika kungoja mpaka walipotimiza miaka 18 ili kuingia rasmi mkataba na klabu hiyo .