Mfanyabiashara, Elizabeth Balali (54) ambaye anadaiwa kuwa Msimamizi wa Mali za Mke wa marehemu Daud Balali, mkazi wa Boko Magengeni, Dar es Salaam amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kesi ya kujipatia Sh.Mil 25 kwa njia ya udanganyifu.
Wakili wa serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amemueleza Hakimu mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina kuwa kati ya Oktoba 19 na Desemba 21, 2017 Dar es Salaam mshtakiwa alijipatia kiasi cha Sh.Mil 25 kutoka kwa Dk.Roderick Kisenge kwa njia ya ulaghai akijifanya anamuuzia eneo lenye ukubwa wa square mita 900 ambalo halijapimwa lililopo eneo la Boko Dovya Kinondoni wakati akijua kuwa eneo hilo si lake.
Pia anadaiwa siku na mahali hapo hapo mshtakiwa huyo alipokea kiasi hicho cha Sh. Mil 25 kutoka kwa Dk. Kisenge kupitia akaunti yake iliyopo kwenye benki ya CRDB wakati akijua fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Elizabeth hakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikilizwa makosa ya Uhujumu Uchumi na pia shtaka la utakatishaji wa fedha halina dhamana.
Upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika, ambapo kesi huyo imeahirishwa hadi Oktoba 24, mwaka huu 2019 kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa amepelekwa rumande.
RC MWANRI AMVUNJA MBAVU RAIS MAGUFULI KWENYE MKUTANO, AMUELEZEA TORONTO YA TABORA