Mkoa wa Mbeya umekumbwa na ajali mfululizo hivi karibuni mpaka kupelekea Viongozi wa dini na Wazee wa kimila kufanya maombi kulikemea zimwi hilo ambapo ikiwa ni siku chache baada ya maombi hayo, ajali nyingine zimetokea usiku wa kuamkia leo.
Usiku wa kuamkia leo gari aina ya Land Cruiser limeigonga Bajaji na kusababisha vifo vya watu watatu kwenye eneo la Kadege usiku wa kuamkia leo ambapo usiku huohuo gari aina ya Toyota Hiace imewaka moto ikiwa barabarani katika eneo la Mbembela ambapo Dereva na Kondakta waliokuwemo ndani yake wamenusurika.
Ikumbukwe kuwa baada ya ajali iliyotokea katika mteremko wa Mbalizi, Waziri Mpya wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alitangaza kuyavunja mabaraza ya Usalama Barabarani ya Mikoa na Wilaya zote nchini.
Waziri huyo pia alimshusha cheo aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani (RTO) wa Jiji la Mbeya, Leopold Fungu hadi kubaki na nyota 3 ambapo baada ya hatua hizo, ajali nyingine ilitokea katika mteremko wa Igawilo na kuua watu watano na kujeruhi mmoja.