Wananchi na Wakulima katika Halmashauri ya wilaya ya Mbogwe Mkoani Geita wamewalalamikia viongozi wao wa kata kwa kushindwa kudhibiti Baadhi ya watumishi wa Halmashsuri hiyo ambao wamekuwa wakikamata wakulima wanapokuwa wanavuna Mazao huku wakiwataka kulipia ushuru wa Mazao ya chakula.
Hayo yamebainishwa katika kikao cha uwasilishaji Taarifa ya utekelezaji wa Irani ya CCM kwa kipindi cha Mwezi Julai mpaka Disemba 2023 wilayani humo Baada ya viongozi na Madiwani kulalamika juu ya kuwepo kwa Kamata kamata kwa Waendesha Pikipiki wanaopakia Gunia tau na Baadhi ya wakulima huku serikali ikishikiza wakulima hao kulipa ushuru wakati wa kusafirisha mazao yao yanapotoka shambani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbogwe Bw. Mathias Nyororo amesema suala la kulipa kodi na ushuru ni suala la kisheria huku akitaka Busara itumike katika kuishauri serikali namna ya kuchukua ushuru huo.
Mkuu wa wilaya ya Mbogwe Bi. Sakina Mohamed amesema hayuko tayari kuacha wilaya yake ikipoteza Mapato kutoka kwa wafanyabiashara ambao wamekuwa wakifanya biashara na kutokulipa ushuru huku akikanusha juu ya kuwepo kwa wakulima ambao wametozwa ushuru wakiwa wanayasafirisha mazao ndani ya wilaya.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbogwe Nikodemas Maganga amewaonya baadhi ya watoza ushuru ambao wamekuwa wakitumia Jina la Mh Rais .Samia Suluhu Hassan vibaya kuwa Kipindi anafanya ziara aliagiza halmsahauri kutoza ushuru kwa mkulima ambaye mazao yake yako chini ya tani moja jambo ambalo sio kweli.