Staa wa Simba SC Clotous Chama raia wa Zambia ameamua kutolea ufafanuzi sakata lake la kudaiwa kuwa yeye ni mtovu wa nidhamu na amechelewa kwenda kuungana na timu ya taifa ya Zambia makusudi huku akiachwa na ndege mara mbili, Chama aweka kupitia Instagram account yake.
“Ningependa kuongelea upande wangu kuhusiana na wito wangu kwa timu ya taifa (Zambia), hususani kuhusiana na suala na mpangilio wa safari yangu, sikuwa nataka kuzungumza chochote kuhusiana na hili lakini nafikiri kuna ulazima wa mimi kufanya hivyo”
“Kwanza wote mnahitajika kujua mimi na kocha (Micho) kwa pamoja na chama cha soka Zambia (FAZ) tuko katika maelewano mazuri, sikuwa na muda wa kumsikiliza kocha leo kuhusiana na press yake na waandishi lakini nimezungumza yote kuhusiana na masuala haya na meneja wa timu ya taifa”
“Ukweli ni kwamba sijaachwa na ndege mara mbili na nilizungumza na kocha kabla ya mchezo wetu Dodoma (Simba vs JKT Tanzania) na kumueleza kwamba sitaweza kusafiri katika ratiba ya ndege ya kwanza niliyokuwa nimepata saa 9 alfajiri Jumatatu wakati mchezo wetu ulikuwa Jumapili saa 10 jioni Dodoma”
“Umbali kutoka Dodoma hadi Dar es Salaam ni saa nane kwa barabara na timu haikuwa imetuandalia usafiri wakurejea mapema Dar es Salaam baada ya mechi, nilipata tiketi yangu ya ndege ya pili leo na muda wa kuondoka ilikuwa ni saa 2:45 asubuhi wakati najiandaa na safari nikaambiwa sitaweza kusafiri majira ya saa 9 jioni”
“Sikubaliani na Wazambia wengi ambao wamekuwa wakiamini kuwa sina nidhamu lakini pia sikuachwa na ndege zote mbili nilizokuwa nimepata kama ilivyokuwa inasemwa”