Tunayo stori kutokea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, SSP Gerald Ngiichi ameieleza mahakama hiyo kuwa aliamuru askari kupiga risasi hewani kwa ajili ya kutawanya maandamano ya viongozi na wafuasi CHADEMA.
Ushahidi huo ambao wa kwanza kutolewa katika kesi hiyo, SSP Ngiichi alidai kuwa aliamuru risasi zipigwe kwa sababu njia ya kutumia mabomu ya Moshi ‘Machozi’ ilishindikana kuwatanya.
Pia amedai baada ya kuamuru risasi zipigwe hewani na utekelezaji kufanyika, kulitokea sauti kubwa ambayo ilifanya waandamanaji wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kukimbia ambapo amesema hakujua kama Mbowe alikuwa na mbio kiasi kile.
Pia amedai, baada ya waandamanaji kusambaratika, alifanya tathmini na kubaini kuna majeruhi wawili ambapo alikuwepo Akwilina aliyewahishwa Hospitali ya Mwananyamala na baadae kuripotiwa kuwa amefariki.
Ngiichi ambaye ni Ofisa Operesheni wa Kipolisi Kinondoni, na shahidi wa kwanza wa upande wa mashitaka katika kesi ya uchochezi inayowakabili vigogo tisa wa chama hicho ameyaeleza hayo wakati akitoa ushahidi wake dhidi ya kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 13, 14 na 15, 2019 kwa ya kuendelea kusikilizwa.