David de Gea anaweza kuwa ameichezea mechi ya mwisho Manchester United baada ya taarifa kuwa anaweza kurejea Hispania kujiunga na Real Madrid kuzidi kushika hatamu.
De Gea alipata maumivu na kutoka nje ya dimba katika mchezo wa sare ya 1-1 vs Arsenal katika dimba la Old Trafford na inaonekana hatoweza kuichezea United mechi ya mwisho msimu huu dhidi ya Hull jumapili ijayo.
Kocha Louis van Gaal amekiri kwa mara kwanza kwamba nafasi ya kurudi Madrid, mahala ambapo alizaliwa na sehemu ambayo mchumba wa mchezaji huyo Edurne Garcia anaishi, inaweza kuwa ngumu sana kwa De Gea kuikataa pamoja na United kumpa ofa ya mkataba mnono wenye thamani ya £200,000 kwa wiki.
Mkataba wa David De Gea na United umebakiza muda wa mwaka mmoja na kwa muda mrefu sasa Real Madrid wamekuwa wakimzengea kipa huyo na sasa vyombo vya habari vya Hispania vinaripoti kwamba ni suala la muda tu limebakia kabla mchezaji huyo hajasaini Madrid.
Van Gaal alisema: ‘Nimefuatilia suala hili kwa upande wake, yeye ni mhispaniola, mchezaji wa timu ya taifa ya nchi hiyo na sasa anaitaka nafasi ya kwanza kikosini mbele ya Iker Casillas, hivi sasa klabu kubwa ya Kihispania inamtaka, mchumba wake pia ni mhispania, wazazi wake pia wahispania, na huwa wanakuja hapa kila wiki au kila baada ya wiki, hili suala ni gumu kwake.
‘Hatoweza kuondoka hapa kwetu kwa sababu hii klabu kubwa, lakini pia anaweza kwenda kwenye klabu nyingine kubwa na uamuzi wa mwisho anao yeye.
‘Tumempa mkataba mnono na hii ni kwa sababu tunataka aendelee kubaki hapa, baada ya kuwa na msimu mzuri mwaka huu.’