Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro amefanya mazungumzo na Uongozi wa juu wa Shirika la ndege la Umoja wa Falme za Kiarabu la Emirates kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania ambapo vitaweza kuonwa na abiria wapatao milioni 90.2 wanaosafiri kila mwaka kupitia ndege za shirika hilo.
Pia, vivutio hivyo vya utalii vya Tanzania vitakuwa vikitazamwa na mamilioni ya abiria wa Shirika hilo wakati ndege zitakapokuwa zikiruka (takeoff) katika viwanja mbalimbali duniani.
Waziri Ndumbaro amebainisha alipokutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Shirika hilo Dubai ambalo mbali na kusafirisha abiria milioni 90.2 duniani kote pia husafirisha abiria wapatao milioni 20 ambao huunganisha ndege nyingine.
Katika hatua nyingine, Dk Ndumbaro amesema katika mazungumzo hayo wamekubaliana ziandaliwe makala tano (Documentaries) za kuelezea vivutio vya utalii vya Tanzania ikiwemo Zanzibar, Serengeti, Ngorongoro pamoja na Mlima Kilimanjaro.
” Shirila la ndege la Emirates ni Shirika kubwa sana Duniani lengo letu kama nchi ni kuhakikisha abiria wapatao milioni 90.2 wanaviangalia vivutio vyetu kisha wanavipenda halafu wanatembelea Tanzania” Dk Ndumbaro.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Masoko wa Afrika wa Shirika la ndege la Umoja wa Falme za Kiarabu la Emirates, Badr Abbas amesema Shirika la Emirate lipo tayari kufanya kazi na Tanzania katika kuhakikisha vivutio vya utalii vya Tanzania vinajulikana.