Serikali ya Ethiopia imeanza rasmi kuzalisha umeme wa bwawa kubwa lililojengwa kwenye kijito cha Mto Nile.
Waziri Mkuu Abiy Ahmed ameongoza tukio la uzinduzi Jumapili Feb. 20 ambalo lilishuhudia mojawapo ya mitambo 13 ya Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance (GERD) ikianza kuzalisha umeme.
“Kuanzia sasa, hakutakuwa na kitu kitakachozuia Ethiopia,” alisema Abiy.
Wakati huo huo, mhandisi mkuu alibainisha kuwa bado kuna kazi ya kufanywa.
“Tumeanza kuzalisha umeme, lakini hiyo haimaanishi kuwa mradi umekamilika,” meneja wa mradi wa bwawa hilo, Kifle Horo alisema.
“Itachukua kutoka miaka miwili na nusu hadi mitatu kukamilisha,” Kifle aliongeza.
Mradi huo umesababisha msuguano katika mahusiano baina ya Ethiopia na Misri, ambayo inategemea mto Nile wenye urefu wa kilomita 6,695 (maili 4,160) kwa sehemu kubwa ya usambazaji wake wa maji.
Bwawa hilo linatazamiwa kuzalisha zaidi ya megawati 5,000 za umeme, na kuongeza pato la umeme la Ethiopia mara mbili. Pia litakuwa mojawapo ya mabwawa makubwa zaidi ya kuzalisha umeme katika bara la Afrika mara litakapokuwa linazalisha kwa uwezo wake au karibu na uwezo wake katika mwaka mmoja au miwili ijayo.