Siku mbili baada ya mchezaji wa kimataifa wa England anayekipiga katika klabu ya Everton, John Stones, kuandika barua ya kuomba kuuzwa na klabu yake, hatimaye klabu yake imejibu maombi yake.
Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa jioni ya Alhamisi na mwenyekiti wa klabu ya Everton Bill Kenwright, ombi la mchezaji huyo kuuzwa kwenda Chelsea limekataliwa.
Mabingwa wa Uingereza, Chelsea wameshatuma ofa tatu tofauti kwenda Everton ili kumsajili Stones – walianza na ofa ya £20million, kisha £26m na wiki iliyopita £30m na zote zikapigwa chini, na sasa wanategemewa kurudi na ofa ya nne ya £33m.
Taarifa ya Everton iliyowekwa kwenye mtandao wao inasema: ‘Everton Football Club imekataa rasmi ombi la kuuzwa kutoka kwa John Stones.
‘Tangu lilipofunguliwa dirisha la usajili, tumeshakataa ofa nyingi kutoka kwa vilabu tofauti vya Premier League.
‘John hauzwi na ataendelea kubaki hapa kama mmoja wa wachezaji wetu muhimu wa kikosi cha kwanza’