Mshambuliaji wa klabu ya Monaco Radamel Falcao amesema kifungo cha mechi tatu alichopewa mwanasoka bora wa dunia Cristiano Ronaldo sio cha haki kabisa, na kwamba hii adhabu inaonyesha ujinga na udhaifu wa mfumo wa kamati ya nidhamu nchini Hispania.
Ronaldo ambae ni mshambuliaji wa Real Madrid alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kugombana na wachezaji wawili wa Athletic Bilbao Carlos Gurpegui na Ander Iturraspe wikiendi iliyopita.
Baada ya hapo Ronaldo aliongezewa adhabu ya kufungiwa mechi 3 na chama cha soka cha Spain, mechi moja kwa kitendo cha vurugu na mechi mbili kwa vitendo alivyofanya wakati akitoka, lakini kwa mshangao Falcao anahisi mreno huyo hakustahili hata kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
Anasema “haikuwa sawa kabisa kumpa kifungo hicho, kila mmoja aliona lile tukio na anajua Ronald hakustahili adhabu yoyote….. kwa adhabu hii, hakuna tofauti baina ya mchezaji ambaye hakufanya kosa na aliyerusha ngumi kiukweli. hakuna usawa”
Jana jioni Real Madrid walizidi kuwa pabaya baada ya pingamizi lao la adhabu hiyo kutupwa.