Kundi la kwanza la wananchi waliokuwa wakiishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro limepewa fidia na kuondoka rasmi leo kuelekea Msomera Wilayani Handeni Mkoani Tanga kuanza maisha mapya.
Kundi hilo la familia 27 kati ya 103 zilizokubali kuondoka kwa hiyari kwenye hifadhi hiyo, lilitoka jana hifadhini na kufikia mji wa Karatu, Arusha kabla ya kuanza safari alfajiri ya leo kuelekea kwenye makazi yaliyoandaliwa na serikali.
RC Arusha, John Mongella, aliyeongoza zoezi la kuwapa hundi za fidia wananchi hao wa jamii ya kimasai, mbali na kusifia zoezi hilo kuwa ni la kihistoria, amesema ni endelevu litakalohusisha familia zingine zinazoendelea kujiorodhesha.
“Siku hii itakuwa ni leo tu zingine zitakuwa tofauti. Pili nimshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa imani yake na sisi kwa umoja wetu kutuamini viongozi wa Mkoa, Wilaya ya Ngorongoro, Wizara ya Maliasili na Utalii, Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro, viongozi wote wa Wilaya ya Ngorongoro na Mkoa wa Arusha, viongozi wa Serikali na wa kisiasa” Mongella
“Viongozi wa kimila na jamii nzima na nisiwasahau kabisa wanahabari tusiposema kwamba kwa baraka za Rais leo tunaweka historia hii tutakuwa hatundei haki lazima tumshukuru sana kwa hilo. Niwashukuru sana wananchi kwa ujumla wao wote, hawa ndugu zetu leo wanaondoka na wale ambao bado lakini wamejiandikisha na ambao hawajajiandikisha wote wanamchango wao kwenye kufanikisha hili” Mongella
“Niseme tu Mwenyezi Mungu katubariki hili limefanikiwa na mnajua wengine hatujakaa muda mrefu ni kama mwaka mmoja na ushee lakini jambo hili lina miaka mingi na mjadala wake ni wa miaka mingi, kuna mafaili na mafaili yamejaa, kila aina ya ushauri wa kitalaaam na wakawaida umetolewa mpaka leo tumefika hapa,” Mongella