Serikali imesema kuwa hakuna upungufu wa chanjo kwa akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano na kwamba chanjo hizo zipo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na hospitali na kwamba zinatolewa bure bila malipo .
Akizungumza na wataalam wa afya katika Kituo cha Afya Kaloleni Halmashauri ya Jiji la Arusha Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi amesema taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu upungufu wa chanjo hazina uhalisia na kwamba chanjo iko ya kutosha katika vituo vyote vya kutolea huduma za Afya nchini .
Dr. Subi amesema kuwa ni jukumu la wataalam wa Afya kuwahudumia wanawake na watoto bila kikwazo ikiwa ni njia mojawapo yakupunguza na kuondoa kabisa vifo vya akina mama na watoto nchini .
Pia ameagiza Waganga wakuu wote nchini kuhakikisha wanaweka Televisheni na vipeperushi katika vituo vya kutolea huduma za Afya hususani katika majengo wanayohudumia akina mama wajazito na kuweka vipindi vinavyoelimisha akina mama juu ya afua mbali mbali za Afya ya uzazi na jinsi ya kujikinga na magonjwa ya kuambukiza na yale yasiyo ya kuambukiza.
“Naagiza Waganga wakuu wote nchini kununua na kuweka Televisheni katika vituo vya kutolea huduma za Afya na hospitali ili kuwapatia fursa akina mama kujifunza afya ya uzazi ikiwa ni njia ya kupunguza vifo vya akina mama wajawazito .” Dkt. Subi.