Leo January 19, 2019 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Hamisi Kigwangalla ameivunja Bodi ya Makumbusho ya Taifa kwa kushindwa kutekeleza maagizo aliyoyatoa mwaka mmoja uliopita kwa bodi hiyo ikiwemo kutengeza Makumbusho ya Marais.
Dk.Kigwangalla amefanya maamuzi hayo kupitia kikao kilichofanyika katika Makumbusho hiyo jijini Dar es Salaam ambapo amesema anaivunja bodi hiyo hadi hapo itakapoundwa bodi nyingine kwa sababu ya kushindwa kutekeleza maagizo.
“Sikagui michakato, nakagua hatua mliyofikia lakini nyinyi kwa mwaka mzima ndio mnafanya mchakato wa viwanja wakati Dodoma wanagawa viwanja bure, kwahiyo nyie hamjafatilia hata hati hamna, hivyo nyie mna bodi isiyofatilia maagizo”amesema.
Amesema kuwa miongoni mwa maagizo aliyoyatoa ni utengenezaji wa Makumbusho ya Marais na Tembo lakini bodi hiyo imeshindwa kutekeleza majukumu yake, wameshindwa kusimamia Menejimenti, hivyo hakuna faida ya kuwa bodi isiyosimamia maagizo ya serikali.