Jarida la Forbes limetoa ripoti ya mabilionea wadogo zaidi kwa mwaka 2021 na kumtaja Kevin Lehmann, raia wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 18 kuwa bilionea kijana namba moja duniani.
Katika orodha hiyo, vijana wote waliotajwa umri wao ni chini ya miaka 30 ambapo jarida hilo limetumia vigezo vya thamani ya hisa wanazomiliki na viwango vya kubadilishia fedha kuanzia March 5, 2021.
Jarida hilo limewachambua wa kwanza hadi wa mwisho kwa kigezo cha umri mdogo bila kujali vipato vyao.
Katika orodha hiyo, Lehmann anatajwa kumiliki utajiri wa Dola 3.3 Bilioni za Marekani zinazomfanya kuwa bilionea mdogo zaidi duniani baada ya kurithi asilimia 50 ya hisa za kampuni ya baba yake ya Drugstores.
Wang Zelong (24), raia wa China anashika nafasi ya pili anamiliki utajiri wa Dola 1.5bilioni baada ya kurithi utajiri wa dola 1.3bilioni za kampuni ya Pigment Production.
Watatu ni Alexandra Andresen (24), raia wa Norway ambaye ana utajiri wa Dola 1.4bilioni, akifuatiwa na Katharina Andresen (25) ambaye ni ndugu yake kila mmoja alirithi asilimia 42 ya hisa katika kampuni ya uwekezaji ya baba yao.
Austin Russell (26), raia wa Marekani anashika nafasi ya tano akiwa na utajiri wa Dola 2.4bilioni kupitia kampuni ya Autonomous Cartech akifutiwa na Gustav Magnar(27), raia wa Norway anayemiliki Dola 4.4bilioni alizopata kupitia hisa za Kampuni ya Fish Farming inayomilikiwa na baba yake.
Andy Fang (28) anashika nafasi ya saba akifuatiwa na ndugu yake Stanley Tang(28), wote ni raia wa Marekani na kila mmoja anamiliki utajiri wa Dola 2bilioni walizopata kupitia kampuni ya Doordash
Anayeshika nafasi ya tisa katika orodha hiyo ni Sam Bankman (29), raia wa Marekani anayemiliki utajiri wa Dola 8.7bilioni akifuatiwa na Jonathan Kwok (29), raia wa Hong Kong anayemiliki utajiri wa Dola 2.4bilioni alizorithi kupitia hisa za kampuni inayomilikiwa na baba yake.