Leo February 6, 2018 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli amezindua Kituo cha Mafunzo Maalum ya Kijeshi kilichopo Mapinga katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani.
Kituo hicho kimejengwa kwa msaada kutoka Jeshi la Ukombozi la Watu wa China kwa gharama ya Shilingi Bilioni 67.87 na kitatumika kutoa mafunzo ya kijeshi ya kisasa yatakayowawezesha askari kukabiliana na vitisho vya kiusalama vya kisasa.
Rais Magufuli ameshuhudia mazoezi ya kijeshi yaliyofanywa katika kituo hicho yakiwemo shambulizi la kutokea baharini, Makomandoo kukabiliana na magaidi na kupiga shabaha kwa kutumia miundombinu ya kisasa.
Akizungumza na Maafisa, Askari na Wananchi waliojitokeza kushuhudia tukio la makabidhiano ya kituo hicho, Rais Magufuli amelishukuru Jeshi la Ukombozi la Watu wa China na Serikali ya China kwa kutoa msaada wa kujengwa kwa kituo hicho na amesema Serikali ya Awamu ya Tano inathamini na kutambua mchango wa China katika Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania.
Rais Magufuli amesema China imeendelea kudhihirisha urafiki na udugu wake na Tanzania kwani licha ya kujenga kituo hicho pia imetoa msaada wa kujenga kituo cha mafunzo ya kijeshi ya anga cha Ngerengere mkoani Morogoro na miradi mingine ya maendeleo ya jamii, na hivyo amemuomba Balozi wa China nchini, Wang Ke kufikisha shukrani zake kwa Rais wa China, Xi Jinping.
Wang Ke na Jen. Yang Jian wamesema China imejenga kituo hicho cha mafunzo maalum ya kijeshi ambacho ni alama nyingine ya uhusiano na ushirikiano wa kirafiki na kidugu kati yake na Tanzania na wameipongeza JWTZ kwa kupata kituo ambacho wanaamini kitatumika kuimarisha Ulinzi na Usalama wa Tanzania na nchi nyingine za Afrika.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo amesema miundo ya kituo hicho inakifanya kuwa kituo cha kimataifa kilicho bora zaidi Afrika Mashariki na Kati kitakachoweza kutoa mafunzo ya kisasa kwa askari wengi na amemuomba, Rais Magufuli kusaidia ujenzi wa daraja la mto Mpigi litakalokiunganisha na barabara ya kwenda Dar es Salaam.
Rais Magufuli amekubali ombi hilo na pia amekubali maombi ya Jen. Mabeyo ya kupeleka maji, umeme na barabara katika eneo ambalo China imekubali kutoa msaada wa kujenga makao makuu ya JWTZ Mkoani Dodoma na ameahidi kuziagiza wizara husika kutekeleza maombi hayo haraka.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Mapinga waliosimamisha msafara wake na kumuomba awasaidie kulipwa fidia kufuatia maeneo yao kuchukuliwa kwa ajili ya miradi, ukiwemo mradi wa ujenzi wa kituo hicho cha mafunzo cha jeshi na kuvunjiwa nyumba zao katika eneo la Makurunge.
Katika majibu yake Rais Magufuli amesema Serikali haiwezi kurudia kuwalipa watu ambao tayari walishalipwa fidia na hawezi kuwatetea watu ambao wamevunja sheria kwa kuvamia maeneo yasiyokuwa yao.
Rais Magufuli pia amesema Serikali ina dhamira ya dhati ya kutekeleza mradi wa bandari na eneo la uwekezaji la Bagamoyo na amewataka watu wote waliolipwa fidia wakati hawakuwa na maeneo warejeshe fedha za Serikali, waliolipwa fidia kuondoka katika maeneo yaliyolipiwa, na kwa wale ambao hawajalipwa fidia waendelee kutumia maeneo yao kwa shughuli zao mbalimbali
“Tunawatia watu umasikini, hii sio haki” –Hussein Bashe