July 27, Mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika Ikulu ya Magogoni Dar es Salaam aliwaapisha rasmi mabalozi wateule 13 kati ya 23 aliowateua Mei mwaka huu.
Miongoni mwa mabalozi wateule walioapishwa ni Hoyce Anderson Temu anayekwenda kuhudumu kama Naibu Mkuu wa kituo Jiji la Geneva, nchini Uswizi.
Balozi Hoyce Temu anayetoka kwenye kada ya uandishi wa habari na ulimbwende ana uzoefu wa miaka zaidi 15 katika masuala ya mawasiliano na mahusiano ya umma akiwa amefanya kazi katika taasisi nyingi yakiwamo Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) na Benki.
Balozi Hoyce Temu akiwa katika mashirika ya Umoja wa Mataifa alifanyakazi kwa ufanisi mkubwa na kuweza kuyaweka mashirika hayo mbele ya wananchi wa Tanzania na serikali akiwa kama mwamvuli kwa Serikali na Umoja huo kwa kukuza mahusiano ya mashirika zaidi ya 23 yalipo chini ya UN.
Kwa kutumia taaluma yake ya mawasiliano aliwezesha agenda za UN za Maendeleo Endelevu (SDGs) kueleweka miongoni mwa Watanzania na hivyo kushirikisha katika mipango mbalimbali ya maendeleo. Kwa kutumia elimu yake ya diplomasia na habari alikuwa msambazaji mkuu wa agenda hizo.
Balozi Hoyce Temu katika shughuli zake za mahusiano amekuwa chachu ya kuunganisha Umoja wa Mataifa na Mabalozi wa mbalimbali kupata misaada ya kimaendeleo ndani ya nchi ikiwa ni tofauti kabisa na miaka iliyopita ya kwamba fedha nyingi zilikuwa zikitumwa moja kwa moja kutoka makao makuu kuja serikali ya Tanzania kama msaada wa UN ambapo kupitia uchangishaji huo (fund raising) ulifanikishwa na Jumuiya ya Umoja wa nchi za Ulaya (EU), Uswidi, Finland na nchini nyingine kupata fedha za ndani na kuwezesha makundi mbalimbali kutambua fursa na kuzitumia.
Uteuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa nafasi hiyo na hata maelezo yake kwanini ameteua watu chini ya miaka 45 na kuangalia utumishi wao katika maeneo mengi yakiwemo waliofanya na mashirika ya UN inaonesha dhahiri kuaminika kwa Balozi Hoyce katika ufanyaji wake kazi.
Pamoja na mashirika ya UN wakati wa ulimbwende alionesha ubunifu wa hali ya juu kwa kuendesha mambo ambayo awali hayakuwapo katika Miss Tanzania hapo awali. Kuanzia kipindi chao walitembelea mikoa yote ya Tanzania akatengeneza harambee za kutafuta fedha kwa ajili ya wahitaji.
Ikumbukwe kuwa Balozi Hoyce Temu alipata taji la urembo wa Tanzania mwaka 1999 na kuiwakilisha nchi katika mashindano ya mrembo wa dunia nchini Uingereza.
Akiwa mlimbwende mwaka 1999 pia aliajiriwa na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) kama Afisa Uhusiano kwa miaka mitatu wakati huo Matron na Patron wa mradi wa Telefood ya FAO ya kukusanya chakula na kusaidia makundi mbalimbali ambapo Matroni na Patroni walikuwa Hayati Rais mstaafu Benjamini Mkapa na Mama Anna Mkapa walisafiri mikoa yote ya nchi kuwafikia makundi ya wanawake mbalimbali kuendesha miradi ya maziwa, mashine na kufuga kuku ambapo wanawake wengi waliondolewa katika umaskini uliokithiri kupita mradi huo huku Balozi Hoyce akiwa kama sektretari wa kamati ya Telefood.
Balozi Hoyce alikuja na wazo la mpango wa chakula kwa kikapu (Baskets for Food) ikiwa moja ya kazi yake wakati wa taji lake na kuwafikia wanawake wa Singida ambapo vikapu vilivyosukwa na wanawake hao vilipelekwa Marekani vikauzwa katika makanisa na magulio mbalimbali nchini humo na fedha kurejeshwa nchini na hivyo kusaidia familia nyingi kuwa na uwezo wa kifedha na kusaidia kaya zao huku vikundi vya akina mama vikiwezeshwa kimtaji na kuwa na uwezo wa kiuchumi.
Mwaka 2011 Hoyce alianzisha kipindi cha kusaidia wahitaji wa Tanzania ambao walihitaji fedha na faraja katika maisha yao.
Kazi za utangazaji wa kipindi cha runinga cha “Mimi na Tanzania” ambacho kwa sasa kinaitwa “Tanzania Yetu” ilimnadi binti huyu kama mwanamke anayejali na kudhihirisha kwamba urembo alioufanya ulikuwa urembo wenye nia na wenye malengo, kusaidia umma.
Kwa mujibu wa takwimu mtandaoni hadi Machi 2016 kipindi hicho kimesaidia watu 1,000 kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Ukiangalia mambo mengi ambayo Balozi Hoyce Temu amefanya nchini kusaidia watanzania unabaini kwamba binti huyu ni tunda halisi la Kitanzania lililoiva katika anga ya Kidiplomasia na mahusiano ya umma.
Kwa uzoefu wa miaka 15 katika Diplomasia, Balozi Hoyce Temu bila shaka anaenda kufanya vyema kwenye majukumu yake hayo mapya pamoja na kuwa chachu ya kuitambulisha Tanzania duniani akiendeleza kasi yake aliyofanya akiwa katika Mashirika ya Umoja wa Mataifa wakati akifanyakazi nao kutoka hapa nchini.
Ifahamike kazi kubwa ya Ubalozi wa Tanzania mjini Geneva ni kuhakikisha kwamba inaendeleza mahusiano mazuri na Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa yaliyopo Geneva na Vienna Austria.
Pamoja na kuwezesha Tanzania kujulikana pia kama alivyoagiza Rais Samia katika hotuba yake ya kuwaapisha watakuwa na kazi kubwa ya kuhudumia watanzania wanaoishi Uswizi wakiwemo dayaspora na wakazi wa Uswizi ambao wanataka kuja nchini Tanzania katika masuala mbalimbali ikiwemo Utalii, Uwekezaji na masuala mengine ya Kidiplomasia.
Katika hotuba yake Julai 27 mwaka huu, mambo mengine ambayo Rais alisisitiza na mabalozi vijana kutumia uwezo wa vijana katika dunia yenye mabadiliko mengi kusimamia ushindani katika masuala ya uchumi ambayo sasa yapo kitehama zaidi.
Julai 27 Mabalozi hao wanaoenda vituoni wametakiwa kusimamia Utalii, kulinda rasilimali, kukuza uhusiano na mahusiano ya kiuchumi, ‘digital revolution’, kuwezesha utalii wa tiba, na mengine mengi na kutokana na uzoefu wake na elimu yake bila shaka Balozi Hoyce Temu atawakilisha ufanisi na kasi kubwa kutokana na umri wake.
Kwa mujibu wa kitabu cha ‘Nayakumbuka Yote’ cha Balozi Hoyce Temu cha mwaka 2007, ukurasa wa kwanza wa kitabu hicho inaeleza kuwa alizaliwa Hospitali ya Mount Meru Mkoa wa Arusha, Machi 20 ,1978.
Alipata elimu yake ya awali na Msingi Mkoani Moshi katika shule ya msingi Matemboni Old Moshi ambako alisoma mpaka darasa la sita na kuhamishiwa shule ya Arusha ambako alifanya mtihani na kufaulu kuingia shule ya sekondari Arusha na shule kidato cha sita na tano kusomea shule ya Wasichana ya Zanaki Jijini ya Jijini Dar es Salaam.
Alipata Digrii yake ya kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Arizona State cha nchini Marekani.
Baada ya kumaliza shahada ya kwanza alifanya kazi kama Meneja mahusiano na mawasiliano katika Benki ya Standard Chartered na kisha kuchukua Post graduate diploma katika Chuo cha Diplomasia, Dar es salaam.
Baada ya kumaliza alijiunga katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine na kuchukua Digrii ya Mawasiliano ya Umma na sasa yupo mwaka wa 4 katika masomo ya PHD ya mawasiliano Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine.
Kuna tuzo nyingi zimekwenda kwa Balozi Hoyce kabla ya uteuzi wake kuwa balozi. Miongoni mwa tuzo hizo ni ya Uhuru wa Vyombo vya Habari iliyotolewa na UNESCO, Mei Mwaka huu wa 2021.Alipata tuzo ya Super Woman kipengele cha afya, tuzo ya ‘Humanitarian of the Year’, tuzo ya Malkia wa nguvu 2017 na Tuzo ya Mwanamke wa mwaka 2020 iliyotolewa na Efm kupitia kipindi cha Mwanamke cha Dina Marios.
Pamoja na tuzo hizo inatosha kuandika hapa kwamba mwaka 2014 Siku ya Wanawake Duniani taasisi ya MISA ilimtangaza kama moja ya wanawake mashuhuri wanaokuja kwa kasi na wa kuangaliwa. Na baada ya miaka saba Taifa la Tanzania linampa kazi ya kuiwakilisha katika balozi, kwenye kituo ambacho kina pilikapilika nyingi za mahusiano ya kimataifa cha Geneva, Uswizi baada ya mji wa New York, Marekani.