Majaji wa mahakama ya Kimataifa ya jinai ICC wamemchagua Jaji Joyce Aluoch kuwa naibu wa kwanza wa Rais katika mahakama hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu.
Kwenye uchaguzi uliofanyika leo jaji kutoka nchi ya Argentina Silvia Fernández de Gurmendi amechaguliwa kuwa Rais huku Kuniko Ozaki kutoka Japan kuchaguliwa kuwa makamu wa pili wa Rais ambapo mahakama ya ICC inamjumuisha Rais na manaibu wawili wanaotoa muongozo wa mambo katika mahakama nzima ya ICC.
Jukumu la Rais ni kuwasiliana na vitengo vingine kuhakikisha kwamba upande wa mashtka unashughulikia kesi za dharura kwa kuziwasilisha mbele ya majaji wanao teuliwa kuzisikiliza.
“Ni heshima kubwa kuchaguliwa rais wa mahakama ya ICC. nitafanya kila niwezalo kuhakikisha kwamba jukumu ambalo majaji wenzangu wamenitwika linafaulu.. ninatazamia kufanya kazi kwa pamoja na manaibu Joyce Aluoch na Kuniko Ozaki, majaji wengine jamii ya kimataifa kwa jumla kuendeleza jukumu la ICC la kusaka haki amani na heshima kwa sheria”, asema Rais Fernández de Gurmendi.
Makamu wa Rais wa Kenya William Ruto ni mmoja ya viongozi wa juu Afrika ambao wana kesi zinazoendelea katika Mahakama hiyo huku kukiwa na malalamiko pia kutoka kwa viongozi wengi wa Afrika kulalamikia Mahakama hiyo kunyanyasa viongozi wa Afrika na kufanya wengi kushinikiza nchi za Afrika kujitoa kwenye Mahakama hiyo.