Italia imeipiku Uingereza na sasa ndilo taifa lenye idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na virusi vya corona barani Ulaya. Hapo jana nchi hiyo iliandikisha vifo 484 hiyo ikiwa idadi ya chini zaidi ya vifo vya siku moja nchini humo katika kipindi cha kama mwezi mmoja hivi.
Lakini licha ya hilo idadi hiyo imeipelekea idadi jumla ya vifo kufikia 64,520 ikilinganishwa na Uingereza yenye vifo 64,267 kulingana na hesabu iliyofanywa na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins.
Idadi zote hizi hazielezei picha kamili ya hali ilivyo katika nchi hizo na inaaminika kwamba vifo vingi havikujumuishwa kwenye hesabu hasa mwanzoni mwa janga la virusi vya corona ambapo wazee wengi waliokuwa wanaishi kwenye nyumba za wazee walifariki ila walikuwa hawajafanyiwa vipimo vya maambukizi hayo.