Mfanyabiashara wa mtandao, Fadhil Mahenge (27) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na makosa matano ikiwemo utakatishaji fedha wa Mil.123 kwa kutumia line za simu 629.
Fadhil ambaye ni miongoni mwa ‘Wazee wa Ile Pesa tuma kwenye Namba Hii’ amesomewa mashitaka yake mbele ya Hakimu Mkazi, Wanjah Hamza na Wakili wa Serikali, Batilda Mushi.
Wakili Mushi amedai kuwa mshitakiwa anakabiliwa na makosa matano ambapo la kwanza anadaiwa kuchapisha taarifa za uongo katika tarehe tofauti kati ya Januari 2017 na Machi 2019 katika mkoa wa Dar es Salaam, Rukwa, Songwe na mikoa mingine.
Inadaiwa alisamba taarifa kwa kusema ‘Tuma Pesa kwenye namba hii’ bila idhini ya aliowatumia.
Kosa jingine ni kusambaza ujumbe bila ridhaa ambapo inadaiwa kati ya Januari 2017 na Machi 2019 ndani ya jiji la Dar es Salaam, Rukqa, Songwe na mikoa mingine alisambaza ujumbe bila ridhaa kwa watu tofauti tofauti kwa kutumia Line ya simu 629 za mitandao tofauti tofauti.
Katika kosa la utakatishaji fedha inadaiwa alilitenda kati ya tarehe na mikoa hiyo ambapo alijipatia Mil.123 wakati akijua ni zao la fedha haramu.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo,mshitakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa kesi hiyo haina dhamana na Mahakama hiyo haina mamlaka ya kumpatia.Upelelezi wa kesi haujakamilika, kesi imeahirishwa hadi Mei 2, 2019.