Jenerali mwandamizi aliyeongoza mapinduzi ya kijeshi hivi karibuni nchini Sudan Abdel-Fattah Burhan amejiteua tena kuongoza baraza tawala la mpito ikiwa ni hatua inayoashiria nia yake ya kuimarisha udhibiti madarakani.
Wengi wa walioteuliwa ni watawala waliokuwa kwenye baraza lililopita.
Hatua hii inachukuliwa katikati ya ahadi zinazotolewa kila mara na watawala wa kijeshi kwamba watarejesha mamlaka kwa serikali ya kiraia, tangu mapinduzi ya Oktoba 25 ambayo yalifuatiwa na maandamano makubwa ya wanaounga mkono demokrasia wanaoshinikiza kurejeshwa kwa utawala huo wa kiraia.
Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo ambaye ni mshirika wa karibu wa Burhan ametajwa kuwa makamu wa rais, pamoja na majenerali wengine watatu waliorejeshwa. Viongozi watatu wa makundi ya waasi waliopigana vita upande wa Omar al-Bashir pia wamejumuishwa kwenye baraza hilo lenye wajumbe 11 na wawakilishi watano toka upande wa kiraia.