Uongozi wa Mkoa wa Mbeya umepongezwa kwa usimamizi mzuri na hatua kubwa iliyofikiwa kwenye mradi wa ujenzi wa jengo jipya la huduma ya wazazi katika hospitali ya wazazi ya Meta.
Aidha, hatua iliyofikiwa ni asilimia 88 kwa miezi 20 tu kati ya 24 iliyokadiriwa kutumika huku hatua hiyo ikiwa imetumia bilioni 6.4 kati ya bilioni 9 zilizotarajiwa ili kukamilisha mradi huo.
Pongezi hiyo zimetolewa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, mara baada ya kutembelea mradi huo ambao unajengwa kwa utaratibu wa ‘force account’.
Dk. Gwajima alisema ameridhishwa na ujenzi huo kwani ni wa viwango na umaliziaji wake ni mzuri na kasi ya ujenzi wake ni nzuri. Hii inaonesha timu ya Mkoa imejipanga vizuri kwenye usimamizi.
“Nimefurahishwa sana na ujenzi huu kwa mkoa wa Mbeya haya ni mapinduzi makubwa katika kuendelea huduma za afya ya uzazi na mtoto, nilikwishakupita hapa miaka ya nyuma hali ilikua tete kwenye jengo la zamani.
“Mkoa mmefanya kazi kubwa na nzuri, jengo linavutia, Mkoa mmetengeneza Kamati makini ya kununua vifaa katika kusimamia dhana ya force account, kwakweli nimefurahi,” amesema Dk. Gwajima.
Amesema hospitali hiyo ikikamilika itakuwa na vyumba 223 kwa ajili ya huduma, vyumba vya upasuaji vitatu, vyumba maalumu (VIP ), wodi ya kujifungua pamoja na wodi ya wagonjwa mahututi (ICU).
“Kwahiyo mama mjamzito akiingia humo ndani kila kitu kitaishia humo hata kama atatakiwa kuwa kwenye uangalizi maalumu,”amesema.