Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imepanga Julai 2 mwaka huu kusikiliza shauri la kesi namba 220 ya mwaka 2018 ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Bernard Membe dhidi ya Cyprian Musiba.
Katika Kesi hiyo iliyoitwa kwa mara ya kwanza Februari 26, 2019, Membe amemshtaki Musiba, Mhariri wa gazeti la Tanzanite na wachapishaji wa gazeti hilo ambapo anawadai Sh. Bilioni 10 kwa kumchafua.
Shauri hilo jana lilisikilizwa mbele ya Jaji Joacquine De Melo ambapo amepanga pia tarehe hiyo hiyo ya Julai 2, 2019 shauri la msingi litatajwa.
Katika kesi hiyo Membe anawakilishwa na Wakili Jonathan Mndeme huku Musiba akiwakilishwa na jopo la mawakili wanne likiongozwa na Wakili Majura Magafu.
Musiba katika kesi hiyo anashtakiwa kwa kumtuhumu Membe kuwa anamhujumu Rais John Magufuli asitekeleze majukumu yake ya kuwaletea wananchi maendeleo huku akidai kwamba mbinu mojawapo ya kukamilisha hujuma hizo ni maandalizi anayofanya kugombea urais mwaka 2020 kupitia CCM.