Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Muhimbili jijini Dar es salaam, imesema imefanikiwa kuokoa shilingi milioni 660 ambazo zingetumika kwa matibabu ya wagonjwa wa moyo endapo wangesafirishwa nje ya nchi baada ya madaktari bingwa wa hapa nchini kufanya tiba ya moyo bila ya kuusimamisha mnamo mwezi huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo,Professa Mohamed Janabi, amesema kuwa jumla ya wagonjwa wa moyo ishirini na wawili walifanyiwa upasuaji katika siku 10 zilizopita ambazo hazikuhusisha huduma ya kusimamisha moyo ikiwa ni mara ya kwanza kwa utaalamu huo kufanyika hapa nchini.
Amesema taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete inatarajia kuongeza huduma za matibabu ya aina hiyo kwa sababu zinapunguza gharama kwa kiasi kikubwa na huchukua muda mfupi kukamilisha upasuaji kuliko ule wa awali ambapo ilibidi mgonjwa apasuliwe kwa kufunua moyo hatua iliyokuwa inatumia muda mrefu wa takriban saa 6.
Naye Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka India,Profesa Subhash Sinha,amesema kuwa kuna haja ya taasisi hiyo kuendana na teknolojia mpya kila inapotokea ili kuongeza ufanisi.
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ilianzishwa rasmi mwaka 2016 kwa lengo la kuwapatia huduma ya matibabu ya moyo wananchi wa ngazi zote ambapo hadi sasa imefanikiwa kuwapatia tiba ya upasuaji moyo ya aina mbalimbali wagonjwa wa ndani na kutoka nje ya nchi wapatao 100 pamoja na maelfu wengine kupata ushauri na maelekezo.