Kocha ambaye ameamua kuondoka kwenye klabu ya Borrusia Dortmund, Jurgen Klopp amethibitisha kuwa hatajiunga na klabu ya Liverpool kama inavyovumishwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari barani Ulaya.
Klopp majuzi aliiongoza Dortmund kwenye fainali ya kombe la Ujerumani ambapo timu yake ilifungwa 3-1 na Wolfsburg akiwa tayari ametangaza kuondoka kwenye klabu hiyo baada ya kuwa nayo kwa misimu 7.
Vyombo vya habari nchini England vimekuwa vikimhusisha na kocha huyo na mpango wa kujiunga na klabu ya Liverpool ambayo kwa nyakati tofauti imetajwa kuwa mbioni kumfukuza kazi kocha wake Brendan Rogers.
Jurgen Klopp amesema kuwa atakaa nje ya mchezo kwa muda akipumzika na kujipanga upya tayari kwa kurudi mchezoni huku akisema kuwa anahitaji kupumzika baada ya miaka saba ya kazi ngumu.
Kocha huyo pia hakuondoa uwezekano wa kujiunga na wapinzani wa Borrusia Dortmund Bayern Munich endapo fursa itajitokeza hapo baadae.