Leo April 3, 2019 Rais Magufuli ameendelea na ziara yake Mkoani Mtwara ambapo ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara ya lami ya Mtwara – Mniwata na ukarabati wa Chuo cha Ualimu Kitangali kilichopo Newala Vijijini.
Barabara ya lami ya Mtwara – Newala yenye urefu wa km. 50 inajengwa kwa gharama ya Bil. 89.6 (fedha zote zimetolewa na Serikali ya Tanzania) ni sehemu ya barabara ya Mtwara – Newala – Masasi yenye urefu wa km. 210 ambayo ikikamilika itapunguza urefu wa barabara ya ukanda wa maendeleo wa Mtwara kutoka kilometa 1,020 hadi kilometa 825.
Akizungumza katika sherehe za uwekaji jiwe la msingi zilizofanyika katika Kijiji cha Naliendele, Rais Magufuli amesema Serikali imedhamiria kukamilisha barabara hiyo na ameiagiza Wizara ya Ujenzi kutangaza zabuni nyingine ya kujenga sehemu ya barabara ya kuanzia Mviwata – Tandahimba – Newala yenye urefu wa kilometa 100.
Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa na mkandarasi DOTT Services Ltd anayejenga barabara ya Mtwara – Mniwata na ameagiza mkandarasi huyo asipewe kazi nyingine mpaka amalize kazi hiyo kutokana na kasi ndogo aliyoanza nayo katika ujenzi wa mradi huo na pia taarifa za kutofanya vizuri katika mradi alioujenga huko Same Mkoani Kilimanjaro.
Baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi huo, JPM akiwa njiani kuelekea Newala kwa gari amesimamishwa na kuzungumza na wananchi wa Nanguruwe, Mtimbwilimbwi, Nanyamba, Kitama ya Kwanza, Tandahimba, Nanyanga, Mahuta na Newala na kuwahakikishia kuwa barabara ya Mtwara – Tandahimba – Newala – Masasi itakamilishwa yote kwa kiwango cha lami na pia Serikali imeamua kutenga Bilioni 160 kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa maji wa Makonde ambao utamaliza tatizo la maji katika sehemu kubwa ya Mkoa wa Mtwara yakiwemo maeneo hayo.
Kwa wananchi wa Nanguruwe ambao wamelalamikia uamuzi wa kuhamisha hospitali ya wilaya na kuipeleka eneo la Mkunwa, Rais Magufuli ameagiza hospitali hiyo ijengwe hapohapo Nanguruwe kama ilivyopangwa awali.
Rais Magufuli amewapongeza wananchi hao kwa juhudi zao za kuzalisha zao la korosho na ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kuifanya Mtwara kuwa kitovu cha Ukanda wa Kusini kwa kutekeleza miradi mikubwa ya kiuchumi ikiwemo ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, upanuzi wa bandari ya Mtwara, upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mtwara na kuimarisha huduma za kijamii zikiwemo kusambaza umeme katika vijiji ambavyo bado havijafikiwa, kujenga vituo vya afya na hospitali na kuimarisha miundominu ya elimu.
Akiwa Mjini Newala, Rais Magufuli amesimama kando ya viwanda viwili vya kubangua korosho vya Micronix System Ltd ambacho kimedaiwa kufanya kazi kwa robo ya uwezo wake na Cashew-nut Factory One ambacho kimenyang’anywa baada ya aliyebinafsishiwa kushindwa kukiendeleza, na ameagiza Wizara ya Viwanda ufuatilie ufanisi wa viwanda hivyo ili kama haviendeshwi kwa tija iliyokusudiwa vichukuliwe na kupatiwa wawekezaji makini watakaofanya kazi ya kubangua korosho kwa uhakika zaidi.
Majira ya jioni, Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ukarabati wa majengo ya Chuo cha Ualimu Kitangali ambao ni moja ya miradi minne inayohusisha ukarabati wa vyuo vya ualimu hapa nchini (mingine ni vyuo vya ualimu Ndala, Shinyanga na Mpuguso) kwa gharama ya shilingi Bilioni 36.475 ikiwa ni ufadhili kutoka Serikali ya Canada iliyotoa shilingi Bilioni 28.275 na Serikali ya Tanzania iliyotoa shilingi Bilioni 8.200.
Rais Magufuli kesho tarehe 04 Aprili atamalizia ziara yake Mkoani Mtwara kwa kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mbonde na kuzungumza na wananchi wa Masasi na baadaye ataendelea na ziara yake Mkoani Ruvuma ambako ataanza kwa kufungua barabara ya lami ya Mangaka – Nakapanya – Tunduru, na Mangaka – Mtambaswala.