Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera, linatarajia kupeleka kwenye Ofisi ya Mashtaka jalada la kesi ya mwanamke Herieth Pontian (27), anayetuhumiwa kumtupa mwanaye wa kumzaa mtoni akiwa hai na hatimaye kufariki, mara baada ya uchunguzi huo kukamilika.
Taarifa hiyo imetolewa hii leo Oktoba 14, 2020, na Kamanda wa Polisi mkoani Kagera Revocatus Malimi, na kusema kuwa kwa sasa wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha uchunguzi na kwamba kucheleweshwa kwa jalada hilo, kumetokana na taratibu za kumpima hali ya afya ya akili, hii ni kutokana na mazingira ya tukio analotuhumiwa kutenda.
Hata hivyo kamanda huyo amekataa kuzungumzia majibu ya vipimo vya afya ya akili vya mama huyo, kwa madai kuwa majibu hayo ni sehemu ya ushahidi utakaotolewa endapo atafikishwa mahakamani.
Mtoto Prince Onesmo mwenye umri wa mwaka mmoja, inadaiwa alitupwa mtoni akiwa hai na mama yake mzazi, na mwili kuonekana ukielea katika mto Kanoni ulioko katika manispaa ya Bukoba, Septemba 2 mwaka huu.