Tunayo stori kutokea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo Mshereheshaji, Emanuel Mathias (34) maarufu kama MC Pili Pili na mwenzake wameachiwa kwa dhamana katika kesi ya kuchapisha maudhui katika mtandao bila kuwa na leseni ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ( TCRA)
Mbali na Mathias, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Heriel Clemence( 25) ambapo wamesomewa mashitaka yao na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando.
Washtakiwa baada ya kusomewa shtaka lao, walikana kutenda kosa hilo na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika ambapo wakili wa utetezi Jebrah Kambole aliwaombea dhamana washitakiwa hao.
MC Pilipili na Clemence wameachiwa huru kwa masharti ya dhamana ya kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua kutoka kwa Mtendaji wa Kata na barua ambayo imepitishwa kwa Mkurugenzi wa Manispaa, anakotokea mdhamini huyo.Kesi imeahirishwa hadi Mei 7, 2019.