Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Hamis Kigwangalla, ameeleza kuwa kwa sasa anaishi kwa hofu na tahadhali kubwa juu ya uhai wake kutokana na kuwepo kwa kundi la watu wanaomuwinda wakitaka kumuangamiza na kudai kuwa tayari amekwishawabaini na hatua stahiki zinafuata.
Kupitia maneno yake aliyoyaandika leo Januari 22, 2020, katika ukurasa wake wa Instagram,na kusema kuwa hajakusudia kufanya mkutano na Waandishi wa Habari, ili kulizungumzia suala hilo na kwamba baada tu ya kuteuliwa kuwa Waziri ulitokea mtafaruko mkubwa juu ya usalama wake hadi Serikali ikampatia ulinzi.
“Team yangu imefanya kazi nzuri, imenipa uthibitisho wa majina ya wanaotaka nichafuliwe ili niondolewe Uwaziri. Bahati mbaya hakuna cha kunichafua nacho, wanapika hadithi za kitoto na kurudia tu, walidhani ningekaidi maelekezo ya Mhe. Rais juu ya mgogoro wa ndani ya Wizara yetu ili Rais achukie aniondoe, wakakwama, sikukaidi” Waziri Kigwangalla.
Waziri Kigwangalla “November 2019 nililetewa taarifa za kutisha, nikaongeza umakini. Team yangu imenisihi nisiweke majina hadharani na kwamba wanawafuatilia wahusika kwa ukaribu na watazijulisha mamlaka kwa hatua stahiki zaidi, watu wa karibu sana na mimi nimewapa mpango na taarifa zote na wanajua cha kufanya endapo chochote kitanitokea.