Zaidi ya watu elfu 1 na 500 wameripotiwa kufa katika kipindi cha miezi 10 tangu kuripotiwa kwa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia Congo, Wizara ya Afya nchini humo imethibitisha.
Katika hatua nyingine vijana waliokuwa na hasira wameripotiwa kuchoma moto vituo vitatu vilivyokuwa vinatoa matibabu ya Ebola pamoja na kuharibu magari ya wagonjwa Jijini Beni.
Mlipuko wa Ebola DRC mashariki ni wa pili kwa ukubwa katika historia.
Shirika la Umoja wa mataifa linaloshughulikia masuala ya watoto, UNICEF linasema mlipuko huu ni wa 10 kutokea nchini DRC na ni mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo na ni wa pili kwa ukubwa kuwahi kushuhudiwa kwenye historia ukiongozwa na mlipuko wa Ebola huko Afrka Magharibi kati ya mwaka 2014-2016.
Kumekuwa na ongezeko la visa vya Ebola katika Jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC, hususani kwenye eneo la Katwa ambapo timu za kukabiliana na mlipuko zimekumbwa na ukosefu wa imani kutoka kwa wanajamii, mlipuko umekwenda hadi maeneo ya Kayina ambako hali ya usalama ni hatarishi, kwa mujibu wa Stephane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
Via RFI