Muanzilishi wa Amazon, biashara kubwa duniani ya mauzo ya bidhaa mtandaoni, Jeff Bezos amepanga kupeleka mwezini chombo cha anga za mbali.
Bezos anayemiliki shirika la utafiti wa anga na urubani lijulikanalo kama Blue Origin amesema wamepanga kurusha mwezinii chombo cha shirika hilo cha chenye uwezo wa kubeba roboti 4 za utafiti.
Chombo hicho kipya kina ukubwa unaoshabihiana na nyumba ndogo, kitarushwa kuelekea mwezini kwa kutumia roketi mpya yenye nguvu kubwa na injini zilizobuniwa upya.
Bezos ambaye pia ni mmiliki wa jarida la Washington Post alitambulisha mfano wa chombo hicho ambacho kitarushwa kuelekea mwezini katika ofisi za shirika la Blue Origin.
Bezos hakufahamisha ni lini haswa chombo hicho kitafanya safari hiyo ya kwenda mwezini, wala hakusema kama chombo hicho kitabeba watu.
Makamo wa rais wa Blue Origin, Clay Mowry, alisema wanataraji ifikapo mwaka 2024 safari za binadamu kuelekea mwezini zitafanyika.
Naye mshauri maalumu wa masuala ya anga wa shirika hilo, Robert Walker, alisema wamepanga kufanya safari zisizojumuisha watu kuelekea mwezini ifikapo mwaka 2023.