Shangwe na furaha vimetawala kwa wafuasi wa CHADEMA, baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kuamuru Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko waachiwe huru baada ya kushinda rufaa yao kuhusu dhamana.
Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Sam Rumanyika ambapo amesema rufaa hiyo nzima nzima inakubaliwa kwani uamuzi wa Mbowe na Matiko kufutiwa dhamana Mahakama ya Kisutu ni sawa na ‘Mtoto Njiti’.
Pia Jaji ameamuru jalada la kesi hiyo lirudishwe Mahakamani Kisutu na kesi isikilizwe kwa haraka sana. Katika hukumu hiyo ilichokuwa takribani saa 1, Jaji Rumanyika amesema ni kinyume na sheria na ni hatari kwa Mahakama kufuta dhamana bila sababu za msingi.
“Hivyo rufaa nzima nzima wameshinda na waachiwe huru mara moja, pia jalada la kesi lirudi Kisutu mara moja ili kesi isikilizwe kwa haraka,“amesema.
Novemba 23, 2018 Jaji Wilbard Mashauri akiwa Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, alifuta dhamana ya Mbowe na Matiko kutokana na kukiuka masharti ya dhamana.