Viongozi wa dunia wameahidi kuchangisha Euro Bilioni 7.4 kwa ajili ya kufanya utafiti na kutengeneza chanjo dhidi ya Virusi vya Corona.
Ahadi hiyo imetolewa kwenye mkutano ulioitishwa na Halmashauri ya Umoja wa Ulaya uliofanyika kwa njia ya video.
Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema mkutano huo ni mwanzo tu wa juhudi ndefu, Umoja wa Ulaya umeahidi kuchangia Euro Bilioni moja.
Ujerumani itatoa Euro milioni 525 na Ufaransa itatenga Euro milioni 500. Nchi nyingine zilizoahidi kuchangia ni pamoja na Norway ambayo si mwanachama wa Umoja wa Ulaya bali ni mwenyekiti mwenza wa juhudi hizo.
Wenyeviti wenza wa mkutano huo ni Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Italia, Japan na Saudi Arabia ambayo kwa sasa ni mwenyekiti wa kundi la nchi za G20. Viongozi wa Marakeni na Urusi hawakushiriki kwenye mkutano huo.
Mpaka sasa watu milioni 3 na nusu wameambukizwa virusi vya corona na zaidi ya laki mbili na elfu arobaini wamekufa duniani kote kutokana na COVID -19.