Wakurugenzi wawili wa Kampuni ya Vinywaji Vikali (BEVCO) akiwemo Raia wa Ufaransa, Melaine Philippe wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wakikabiliwa na makosa 45 ikiwemo utakatishaji fedha wa Sh.Bil 1.6.
Mbali ya Melaine mshtakiwa mwingine ni Ntemi Masanja.
Washtakiwa hao ambao wanakabiliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi namba 87 ya mwaka 2020 wamefikishwa mahakamani hapo na TAKUKURU na kusomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya.
Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali, Maghela Ndimbo ambapo amedai walitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti ambapo wana makosa ya Kughushi, Kukwepa Kodi, Kuwasilisha Nyaraka za Uongo, Kuisababishia hasara TRA na Utakatishaji fedha.
Kosa la utakatishaji fedha wanadaiwa kulitenda kati ya Oktoba 31, 2017 na June 2020 katika maeneo tofauti Jijini DSM ambapo wanadaiwa walimsaidia Samson Rwegasira na Thierry Lefeuvre kujipatia Sh.Bilioni 1.6 wakati wakijua fedha hizo zinatokana na makosa ya kukwepa kodi, kughushi.
Pia kosa la kuisababishia hasara Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanadaiwa kulitenda siku na tarehe kama hizo katika kosa la utakatishaji fedha.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Wakili Ndimbo alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo anaomba kesi hiyo ipangwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo kwa mujibu wa sheria, Hakimu Isaya alisema washitakiwa hawaruhusiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, hivyo washtakiwa wamerudishwa korokoroni na kesi imeahirishwa hadi Desemba 3, 2020.