Wananchi wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wamewashukuru Madaktari Bingwa wa Samia kwa huduma bora waliofikishiwa katika wilaya hiyo ambapo walijitokeza kwa wingi ili kuhudumiwa.
Neema Laizer mama wa watoto watatu, aliyefikishwa Hospitalini hapo Mei 14, 2024 akiwa na tatizo la uzazi pingamizi, amesema ujio huo umemuokoa kusafiri umbali mrefu wa kilomita 140 kufika Arusha mjini ama kilomita 205 kufika mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kupata huduma.
“Nilifika hapa, nikiwa nimepitiliza uchungu lakini nilipokelewa na wakaka na wadada wazuri, wakanipatia huduma na kwa sasa mimi na mwanangu tunaendelea vizuri”. Amesema Bi. Neema.
Kwa upande wake Bi Nanyori Sanare amesema huduma hizo zimeleta muamsho kwani jamii yao huishi katika mazingira ya mbali mbali.
“Sisi jamii ya Kimasai shughuli zetu kuu ni ufugaji, hivyo tumekuwa na desturi ya kuhama hama, kwetu sisi tunamshukuru sana Mama Samia kwa kutuletea Madaktari Bingwa na Bobezi”. amesema Bi Nanyori.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Simanjiro Dkt. Sebaldi Mtitu amesema ujio wa Madaktari Bingwa na Bobezi ni neema kwa Wilaya yao.
“Mei 14 tulipokea mtoto wa mwaka mmoja aliyekuwa amemeza shilingi 200 na kwa kawaida ingebidi tumuandikie rufani ya dharura na kukimbizwa KCMC au Arusha, lakini Madaktari Bingwa hawa waliingia kazini na kufanikisha zoezi la kutoa sarafu hiyo.” Amesema Dkt. Mtitu.
Mtitu amesema mbali ya upasuaji wanaoufanya kwa wananchi lakini pia wamekuwa msaada katika kuwajengea uwezo wataalam walio katika vituo hivyo.
Naye Angelle Titus, Afisa Tabibu ambaye amekuwa bega kwa bega na Dkt. Edwin Masholla anayemjengea uwezo, amesema ujio huo umekuwa ni darasa kubwa kwao kwani hata baada ya kuondoka wataendelea kutumia maarifa watakayo waachia.
Madaktari Bingwa na Bobezi wanaotembea na Kaulimbiu isemayo Tumekufikia Karibu Tukuhudumie wapo wilaya mbalimbali za mkoa wa Manyara wakiwahudumia wananchi kuanzia Mei 13 hadi 17, 2024.