Mabingwa wa ulaya Real Madrid hii leo (jumapili) wameuanza vibaya mwaka 2015 baada ya kukubali kipigo cha 2-1 toka kwa Valencia katika mchezo wao wa 17 wa ligi kuu ya Hispania uliopigwa kwenye uwanja wa nyumbani wa Valencia Estadio Mestalla.
Katika mchezo huo ambao ulikuwa wa kwanza kwa Real Madrid tangu kuanza kwa mwaka mpya Real walianza kwa kasi wakifunga bao kwenye dakika ya 14 mfungaji akiwa Cristiano Ronaldo akifunga kwa mkwaju wa penati baada baada ya mshambuliaji wa Valencia Alvaro Negredo kuushika mpira kwa mkono.
Bao hilo kwa Real Madrid lilidumu kwa muda mrefu kidogo na Valencia walisawazisha mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya dakika 7, kwenye dakika ya 52 mfungaji akiwa Antonio Baraggan ambaye alipiga shuti kali lililowazidi mabeki Sergio Ramos na Pepe pamoja na kipa wao Iker Casillas.
Bao hilo liliamsha mashambulizi ya Valencia na haikuwachukua muda kabla ya kufunga bao la pili mfungaji akiwa beki raia wa Argentina, Nicolas Otamendi ambaye alifunga kwenye dakika ya 65 ya mchezo akimaliza kwa kichwa kona iliyopigwa na Dani Parejo.
Real Madrid walijaribu kusawazisha bao hilo bila mafanikio yoyote na hadi dakika 90 zinamalizika Valencia waliondoka na pointi zote 3.
Huu ni mchezo wa kwanza kwa Real Madrid kupoteza rekodi yake ya kushinda michezo 22 mfululizo huku wakishindwa kuifikia na kuizidi rekodi ya timu ya Brazil ya Coritiba ambayo iliwahi kucheza mechi 24 za kiushindani bila ya kupoteza mechi hata moja.
Ni halali yako kupata kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>> twitter Insta Facebook