Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani Alhaji Majid Mwanga kuwasaka, kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wafugaji wote wanaodaiwa kuhusika katika matukio ya kuwashambulia kwa viboko wananchi wa Kijiji cha Fukayosi kilichopo Wilayani humo.
Dkt. Magufuli aliyekuwa akisafiri kwa gari kutoka Dodoma kwenda Jijini Dar es Salaam ametoa agizo hilo leo march 17 2017 aliposimama katika kijiji hicho baada ya kuona wananchi wengi wakiwa wamekusanyika kando ya Ofisi ya Kata.
Baada ya kusimamisha msafara wake, Rais Magufuli aliwaita wananchi waliokuwa wamekusanyika huku wakiwa wameshika mabango yaliyoandikwa ujumbe wa kutaka wafugaji wa jamii ya Wamang’ati waondolewe na kisha akatoa nafasi kwa baadhi yao kueleza dukuduku lao.
Wananchi hao ambao ni wakulima na mfugaji mmoja aliyejitokeza wakaeleza kuwa Wamang’ati wamekuwa wakiwanyanyasa kwa kuingiza mifugo katika mashamba yao ya mazao na wakithubutu kuwakataza wamekuwa wakichapwa viboko na baadhi kuuawa.
Katika majibu yake, pamoja na kutaka wote wanaodaiwa kuwashambulia wananchi kwa viboko wakamatwe Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo kukomesha mara moja vitendo vya wafugaji kuwapiga wakulima na wakulima kuwapiga wafugaji, na pia kukomesha vitendo vya wafugaji kulisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima.
“Kuanzia leo isitokee mfugaji kumpiga mkulima, mkulima kumpiga mfugaji wala mfugaji kulisha mifugo yake kwenye mashamba ya wakulima na suala hili nitalifuatilia mimi mwenyewe.
“Kwa hiyo Mkuu wa Wilaya na Viongozi mlishughulikie hili kabla mimi sijawashughulikia nyinyi, wale waliopiga watu, nataka wote wakamatwe na wafikishwe kwenye vyombo vya sheria”
Ulikosa? Rais Magufuli alivyofuta agizo la cheti kwa watakaofunga ndoa, Bonyeza play hapa chini kutazama