Mahakama Kuu nchini Nigeria imeamuru kuwa ukahaba si kosa kwa kuwa hakuna sheria yoyote nchini humo inayozuia kitendo hicho. Uamuzi huo umetolewa jana na Jaji Binta Nyako wa Mahakama Kuu jijini Abuja akiamuru wanawake 16 waliokamatwa mwaka 2017 kwa kufanya ukahaba walipwe fidia.
Kwa mujibu wa BBC, hii ni mara ya kwanza kwa mahakama nchini Nigeria kutoa hukumu ya aina hiyo kuhusu uhalali wa ukahaba.
Wakili wa washtakiwa hao, Babatunde Jacob aliieleza BBC kuwa mahakama imeonyesha kuwa vyombo vya usalama vilikiuka haki ya wateja wake kwa kuvunja nyumba na kuwakamata wakisema ni makahaba.
Wanasheria wanaamini kuwa hukumu hiyo inaweza kuwa na athari kubwa zaidi katika nchi hiyo ambayo ni kawaida kwa vyombo vya dola kuwakamata makahaba.
Katika tukio mojawapo mwezi May, zaidi ya wanawake 60 walitiwa mbaroni kwa kujihusisha na ukahaba.