Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema kwamba hakuna laini ya simu itakayofungwa kabla ya Desemba 31 na hivyo wananchi wanatakiwa kwenda kusajili laini zao kwa kutumia Vitambulisho vya Uraia kwa kuwa hakutakuwa na mabadiliko ya muda wa kuzifunga.
Kaimu Meneja Mawasiliano wa TCRA, Semu Mwakanjala, amesema hadi sasa laini za simu milioni 20 zimesajiliwa na ikifika Desemba 31, 2019 laini zote ambazo hazijasajiliwa kwa Namba ya NIDA na kuthibitishwa kwenye mifumo zitafungwa.
Aidha, amesema hakuna mtoa huduma atakayeruhusiwa kufunga au kukatisha mawasiliano ya mtumiaji yeyote kabla ya muda uliopangwa.
Ufafanuzi huo umetolewa baada ya baadhi ya watumiaji wa laini za simu kuanza kulalamika kukosa mawasiliano kwenye baadhi ya laini kwa kile kilichoelezwa kuwa zimezimwa kwa kuwa hawajasajili.